Wanasoka wa5 matajiri Afrika wenye mioyo ya kusaidia jamii

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:10 PM Jul 01 2024
 Sadio Mane.
Picha: Mtandao
Sadio Mane.

SOKA ni mchezo pendwa duniani, unatajwa kufuatiliwa na watu zaidi ya bilioni nne, ukiingiza mabilioni ya dola kwa wachezaji na watu wengine wanaoshughulika na soka. Ukitaja wanamichezo wanaolipwa pesa nyingi duniani, wacheza soka ni miongoni mwao.

Ukiacha malipo ya mishahara wachezaji wa soka wengi wanapata fedha kutokana na matangazo ya kibiashara na haki ya kutumika kwa sura zao.

Ukweli ni miongoni mwa binadamu wanaoishi kifahari ikiwamo kununua majumba mazuri, magari mazuri ya kifahari, ndege na anasa zingine.

Kuwa na fedha ni jambo moja, kuwa na moyo wa kurudisha ulichovuna kwa jamii ni jambo lingine. Wapo wachezaji wa sasa na waliostaafu wenye mioyo ya kutumia fedha zao na umaarufu wao kusaidia jamii.

Cristiano Ronaldo, Mesut Ozil, David Beckham, Lionel Messi, Riyad Karim Mahrez , Mario Balotelli, Yakubu Ayegbeni, Neymar na Marcus Rashford ni miongoni mwa wanasoka wachache duniani wenye mioyo ya kipekee ya kusaidia jamii kwenye maeneo tofauti tofauti. Kwa bara la Afrika wafuatao ni wanasoka watano wanaotajwa kuwa na mioyo ya kipekeee ya kusaidia jamii zao. 

1: Mohamed Salah

Walemavu ni miongoni mwa makundi yanayosaidiwa sana na Mo Salah

Salah ni mmoja kati ya wachezaji bora duniani, akiwa anapokea mshahara mkubwa zaidi katika klabu yake ya Liverpool akipokea zaidi ya dola milioni 14 kwa mwaka. Kama ilivyo kwa nyota mwenzake wa Liverpool, Sadio Mane, pia hajasahau alipotoka, nchini Misri. Mo Salah alitoa maelfu ya mitungi ya oxygen kwenye hospitali za Misri kwa ajili ya kukabiliana na janga la corona.

Mwaka 2019, alichangia dola za Kimarekani milioni tatu sawa na Sh. bilioni 8.2 za Tanzania, kwenye taasisi ya kansa nchini Misri, ili ifanye ukarabati wa miundombinu yake baada ya kushambuliwa na magaidi.

Mwaka 2018, alitumia dola karibu nusu milioni kusaidia kununua eneo kubwa la kujenga mradi wa maji katika kijiji chake cha Nagrig. Mbali na hiyo ana miradi mingi ya kusaidia watu katika kijiji hicho na Misri kwa ujumla ikiwamo kuanzisha Taasisi ya Misaada ya Al-Azhar na kituo kikubwa cha huduma za magari ya wagonjwa wa dharura (Ambulance). 

2: Samuel Eto'o

Huyu anatajwa kama mchezaji wa muda wote wa Afrika. Mshambuliaji huyu wa zamani wa Timu ya Taifa ya Cameroon na klabu kubwa kama Barcelona, Chelsea na Inter Milan, mbali na kuonyesha dunia uwezo wake wa kusakata kabumbu uwanjani, anaonyesha utu wake pia nje ya uwanja.

Amejielekeza zaidi kutimiza ndoto za watoto na vijana wengi kwenye maisha yao, mbali na kusaidia huduma za msingi kama malazi na chakula, amekuwa akiwasaidia pia kupitia kuwafadhili kwenye masomo yao. Ameshiriki kwenye miradi mingi ya kusaidia miundombinu ya afya barani Afrika. 

3: Sadio Mane

Mchezaji bora wa Afrika mwaka 2019, ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi akipokea zaidi ya dola milioni 10 kwa mwaka. Anatajwa kama mwanasoka mwenye utu zaidi kwa sasa. Utu wake ukijengwa zaidi na alivyoshikilia dini kwa imani yake ya kiislamu.

Hatumii fedha yake yoyote kwa ajili ya starehe, anaishi kama mtu mwenye pesa, lakini si kifahari kama wachezaji wengine wa Afrika. Pesa yake nyingi anairejesha nyumbani kwao Senegal na familia yake.

"Kwa nini nitake kununua magari 10 ya Ferraris, saa 20 sa almasi au ndege mbili? Hivi vyote vitanisaidiaje mie na dunia? Aliwahi kunukuliwa hivi karibuni akisema

"Nimeishi maisha magumu ya kimasikini, nimecheza mpira bila viatu utotoni, sijasoma mie, lakini leo navuna fedha nyingi , asante soka, sasa naweza kusaidia watu wangu."

Anaishi katika maneno yake, ukiacha michango ya kawaida anayotoa katika maeneo mengi ya Afrika, Mane amejenga shule kijijini kwao, Bambuli Senegal, amejenga hospitali kubwa na msikiti mkubwa wa kuabudia jamii yake. 

4: Didier Drogba

Ukiwataja wanasoka waliowika zaidi kwenye soka Afrika katika miaka ya hivi karibuni, huwezi kumuacha mshambuliaji huyu wa zamani wa Chelsea na Timu ya Taifa ya Ivory Coast. Ni gwiji aliyeanzisha taasisi yake ya Didier Drogba Foundation, ambayo imejenga hospitali kadhaa, shule na vituo vya kusaidia watoto yatima.

Moyo wake wa huruma unakumbukwa zaidi mwaka 2007 alipomaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini mwake iliyodumu kwa zaidi ya miaka mitano. Moyo wake wa kusaidia hauishii tu nchini kwake, zaidi ya nchi 10. 

5: Nwankwo Kanu

Mashabiki wa Nigeria na Arsenal wanamfahamu sana huyu, akiwa sehemu ya kikosi cha Arsenal kilichoshinda taji la Ligi Kuu England msimu wa 2003/2004 bila kupoteza hata mchezo mmoja 'Invincibles'.

Kanu aliyewahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mara mbili, anatajwa kuwa na utajiri wa dola milioni tisa, uliotokana na soka.

Ameamua kurejesha utajiri wake kwa jamii kwa kuanzisha moja ya hospitali kubwa ya moyo Afrika na kurejesha tabasamu kwa Waafrika wengi. Kanu Heart Foundation ilianzishwa mwaka 2000 akiwa bado mchezaji wa Arsenal baada ya kupata tatizo la moyo, akiwa mchezaji. Mpaka sasa maelfu ya watoto katika nchi za Afrika Magharibi wamenufaika na mradi huo.