Iddi Azzan afunguka kuhusu Chama Yanga

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 12:03 PM Jul 03 2024
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Iddi Azzan.
Picha: Maktaba
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Iddi Azzan.

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Iddi Azzan, amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kutohuzunika kwa sababu ya kuondoka kwa kiungo mshambuliaji wao, Clatous Chama, ambaye ametangazwa kujiunga na watani zao, Yanga.

Chama ameondoka Simba baada ya kumaliza mkataba wake Juni 30, mwaka huu, kutokana na klabu hiyo kushindwa kumpa kiasi cha fedha alichohitaji ili kubakia klabuni hapo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Azzan alisema Chama si mchezaji wa kwanza mkubwa kuihama klabu hiyo na kwa sasa mpira ni Biashara, hivyo wachezaji wana uhuru wa kufanya uamuzi wapi watacheza kwa msimu husika.

Azzan alisema anaamini Simba itapata mchezaji mwingine mwenye kiwango bora zaidi ya Mzambia huyo na viongozi waliamua kuachana naye kwa kuzingatia maslahi ya klabu na si vinginevyo.

"Chama alikuwapo Simba na kuitumikia kwa kipindi kirefu tu,  akanunuliwa Morocco, akarudi tena Simba, lakini sasa ameondoka, tuwaamini viongozi wetu kwa maamuzi yao, tuamini watatuletea nyota wakali zaidi na wataisaidia timu kufanya vema," alisema Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Kinondoni (CCM), Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa mazoea ya wachezaji kucheza na 'kuzeekea' katika klabu moja kwa sasa hayapo na hii inatoka na makubalinao yanayofikiwa baada ya kumaliza mkataba wa awali.

"Tutapata mchezaji mzuri kuliko Chama, tukubaliane na uamuzi uliofanywa na viongozi wetu, inawezekana wameona kwa sasa hatumhitaji au hawawezi kumpa kile alichokihitaji, na Yanga wamempa kwa sababu wanaamini atawafaa, " aliongeza Azzan, ambaye ni mwanachama wa 'Wekundu wa Msimbazi' hao.

Simba inaendelea kufanya usajili wake wa wachezaji wapya wa ndani na nje na wameanza kuwasili jijini tayari kwa maandalizi ya kuelekea Ismailia, Misri kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa mashindano.

Hata hivyo, Simba bado haijatangaza rasmi mrithi wa Kocha Abdelhak Benchikha, ambaye aliachana na timu hiyo zikiwa zimebakia mechi chache za msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.