Uwekezaji Bandari Dar waduwaza viongozi UVCCM

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 08:58 PM Jul 05 2024
Uwekezaji Bandari Dar waduwaza viongozi UVCCM
Picha: Mpigapicha Wetu
Uwekezaji Bandari Dar waduwaza viongozi UVCCM

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetembelea maeneo ya uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam, uliofanywa na kampuni ya DP World na kusema uwekezaji huo umeleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji na ufanisi

Akizungumza mara baada ya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM , Mohamed Kawaida aliipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kuruhusu uwekezaji huo ambao alisema una manufaa makubwa kwa taifa.

Alisema ripoti ya utendaji iliyowasilishwa na uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), umeonyesha kuongezeka kwa ufanisi na kazi ya upakuaji na usafirishaji wa mizigo bandarini hapo tofauti na hofu iliyokuwepo hapo awali na watu waliokuwa wanapinga uwekezaji huo. 

“Sisi ni wasimamizi wa Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, tumeamua kutembelea Bandari ya Dar es Salaam kujionea shughuli mbalimbali zinavyofanyika na tumefurahishwa na ufanisi wake baada ya uwekezaji mkubwa,” alisema Kawaida.

 Alisema lengo kubwa la ziara hiyo ambayo pia ilihusisha wenyeviti na makatibu wa umoja wa vijana kutoka mikoa yote hapa nchini, lilikuwa kujionea na kujifunza namna kazi zinavyofanyika bandarini hapo.

“Mimi na viongozi wenzangu wote wa UVCCM tumefurahishwa na tija ya uwekezaji huu katika Bandari ya Dar es Salaam,” alisema na kuongeza kuwa awali kulikuwa  na maneno mengi ya upotoshaji kuwa uwekezaji huo hauna tija kwa taifa na watanzania wengi wangepoteza ajira na wafanyabiashara kukimbilia bandari nyingine za nchi jirani

Alisema mwekezaji DP World amewekeza fedha nyingi katika miundombinu na vitendea kazi hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa  kuongezeka kwa shehena za mizigo katika bandarini hapo.


“Lakini katika ziara hii tumejionea hali tofauti kabisa, ufanisi na upakuaji mizigo umeongezeka baada ya uwekezaji mkubwa wa miundombinu na vitendea kazi kufanyika,”alisema

“Hii inamaanisha kuwa mapato yanayotokana na uwekezaji huu yameongezeka na kuwa na tija katika maendeleo ya nchi yetu,”alisema Kawaida na kuongeza kuwa  Tanzania imepata neema ya kuwa na bandari hiyo inayohudumia nchi mbalimbali zikiwemo Rwanda, Burundi, Congo DRC, Msumbiji na Zambia.

Akizungumza kwa niaba ya  Mkurugenzi ya Mkurugenzi wa TPA, Plasduce Mbosaa, Mkurugenzi  wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Selemani, alisema viongozi wa umoja huo  wamefurahishwa na ufanisi unaofanywa na mwekezaji DP World bandarini hapo kama ilivyotarajiwa na wamejifunza mengi wakati wa ziara hiyo.

Alisema ili kuleta ufanisi na tija, mwekezaji DP World ameweka vitendea kazi mbalimbali bandarini hapo katika kuhudumia shehena za mizigo na kufanya ufufuaji wa mashine zilizokaa muda mrefu bila kufanya kazi.


Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuitumia bandari hiyo kutokana na mageuzi makubwa yanayofanyika katika kuharakisha kazi ya upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini hapo.

Ripoti ya utendaji kazi wa bandari hiyo iliyowasilishwa wakati wa ziara hiyo kwa viongozi wa umoja huo imeonyesha mafanikio makubwa  yamepatikana baada ya Serikali chini ya Rais Samia kuridhia uwekezaji wa DP World bandarini hapo.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2020/21/22/2023), mapato ya Bandari ya Dar es Salaam yamekuwa yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 27.2 kwa mwaka, kutoka kiasi cha shilingi bilioni 801.7 hadi trilioni 1.3 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kulikotokana na kuongezeka kwa shehena zikiwemo kutoka nchi za jirani.