Marekani yashiriki uzinduzi Ndondo Cup 2024 nchini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:08 PM Jul 03 2024
Evangelina Chihoma kutoka Ofisi ya PEPFAR.
Picha: Mtandao
Evangelina Chihoma kutoka Ofisi ya PEPFAR.

SERIKALI ya Marekani kupitia mradi wa Breakthrough Action, mwaka huu imejiunga na wadau mbalimbali nchini kuandaa Ndondo Cup 2024.

Shirika la Maendeleo la Marekani la (USAID) na Mfuko wa PEPFAR, umeipa shavu Ndondo Cup kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, benki pamoja na kampuni nyingine binafsi.

Lengo likiwa ni kusogeza huduma za afya hasa VVU na chanjo kwa wapenzi na mashibiki wa michuano hiyo inayofanyika kila mwaka Dar es Salaam.

Ujio wa Marekani kwenye Ndondo Cup 2024, unafanywa kupitia Kampeni ya Afya ya Vijana ya Sitetereki, ikilenga wanaume kupambana na VVU. 

Kampeni hiyo iliyobeba ujumbe 'Furaha Yangu Chanjo ni Maisha' itabeba mashindano ya Ndondo Cup 2024 yatakayofanyika katika mikoa nane ya Tanzania; Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Kagera, Dodoma, Mwanza na Pwani.

Mashindano hayo yalianza rasmi mwishoni mwa wiki, ambapo ilipigwa mechi ya ufunguzi ya kusisimua kati ya Manzese Warriors na Makuburi FC kwenye Uwanja wa Kinesi uliopo Kata ya Sinza. 

Washiriki walipata huduma kamili za afya, ikiwa ni pamoja na vipimo vya VVU na matibabu na huduma za chanjo ambapo mgeni rasmi alifurahishwa na mpango huu wa ubunifu, akiipongeza kamati ya maandalizi na wadhamini kwa kujumuisha burudani na huduma za afya.

"Tumejitolea kubuni mbinu zinazotoa matokeo halisi ya kiafya," alisema Evangelina Chihoma kutoka Ofisi ya PEPFAR. 

"Tunaamini kwamba michezo inaweza kuongeza nguvu kubwa katika kuleta mabadiliko ya tabia na kuboresha upatikanaji wa huduma, na tunafurahia kushirikiana na Ndondo Cup na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanikisha mashindano haya."

Lulu Msangi, Mtaalamu wa Programu kutoka USAID, aliongezea, "Tunatumia michezo kuhamasisha Watanzania kupata chanjo na kulinda familia zao."

"Mpango huu wa ubunifu utatekelezwa kwenye ngazi ya kitaifa na jamii, ukilenga kuwafikia vijana wanaoshiriki shughuli za kimichezo kupata elimu na huduma za afya hasa zinazohusu VVU na chanjo. Kwa kuingiza huduma za afya katika burudani, mpango huu unalenga upokeaji wa huduma za afya miongoni mwa wavulana na wanaume kwa kutumia umaarufu wa soka."