Serikali zijifunze maandamano na ghasia za kupinga kodi, ushuru

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 12:31 PM Jul 03 2024
 Ghasia za kupinga kodi, ushuru Kenya.
Picha: Mtandao
Ghasia za kupinga kodi, ushuru Kenya.

WATAALAMU wa uchumi na misaada wanakadiria kuwa Afrika imepokea zaidi ya dola trilioni moja za Marekani katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Hata hivyo,  bado hakuna maendeleo na nchi zinategemea misaada kutoka nje ili kujiendesha,  hali inayoashiria kuwa msaada huo hauwafikii wengi na kuzidi kuongeza changamoto za kimaisha.

Aidha, kutokana na kupungua kwa misaada ya fedha kutoka nje, serikali za Afrika zikiwamo za Afrika Mashariki zimeanza  kuminya kila mahali ili kupata fedha, ikiwa kuongeza na kusaka zaidi kodi.

Lakini, tahadhari ni kwamba ushuru unaweza kuwa jambo zuri hata hivyo, wakati viwango vikikithiri  serikali lazima zijue kuwa zinawavunja watu migongo  na huenda ikawa vigumu kupata fedha hizo.

Maandamano  yanayoendelea ya kukataa  kodi yanayotikisa  ukanda wa Afrika Mashariki, huku ghasia na uharibifu wa mali ukionekana nchini Kenya, yanaashiria kuwa namna ya matumizi bora ya kuwaletea maendeleo kutoka kwenye kodi na ushuru  wananchi wanaotozwa ni jambo ambalo huenda limeshindikana na  sasa jamii inaanza kukasirika.

Uhuru wa kujieleza, haki ya kuchukua hatua, kuandamana na kupinga kutozwa ushuru, au kuadhibiwa ukidai haki yako  umeanza kwa miaka mingi  na sasa kizazi cha sasa cha vijana kinauongezea nguvu. 

Kinachoonekana ni kukataa kutozwa ushuru bila kuwa na uwakilishi unaojali shida za raia, wananchi wanataka waone maoni yao yanatumika kwenye kupanga mipango inayoathiri mifuko yao. 

Wanapenda wasikilizwe na maamuzi yanayoathiri taifa. Yaangaliwe kwanza kuliko kuwa na mipango inayoumiza watu kwa manufaa ya wachache.

Kukataa viongozi kufanya maamuzi ya kuumiza wananchi kumekuwapo tangu enzi na enzi na kuna historia zinazozungumzia Mapinduzi ya Ufaransa ambayo yanaelezwa kuwa mfalme na familia yake walikuwa wanakula na kusaza wakati Wafaransa hawana hata maji ya kunywa.

Mapinduzi ya Ufaransa yaliyoanza mwaka  1789 na kudumu hadi 1794, yanaeelezwa kuwa  Mfalme Louis XVI alihitaji pesa zaidi, lakini alishindwa kuongeza kodi zaidi.

Katika changamoto za ugumu wa maisha huko Ufaransa mfalme na Malkia Marie Antoinette, waliuawa 1793, na watu wakimtuhumu malkia kuwa wakati wananchi wanalalamikia kukosa mkate yeye anasema wapewe keki.

Yote hayo yalimaanisha kuwa uongozi haujui uchungu wanaopata walipa kodi na ugumu wa maisha wanayopitia. Si jambo jema kujisahau kama kiongozi kama ilivyotokea kwenye kasri la mfalme wa Ufaransa miaka hiyo.

Kinachoonekana sasa ni kwanza mataifa ya Afrika yajitafakari kwa kuangalia kanuni za ushuru na kodi, je, wananchi wanaweza kuzilipa? Ni nani hasa alipe na yupi asikatwe kodi?  Kulipa kodi ni lazima lakini kunafanywa kwa haki na matumizi yake yakoje? Umma unaridhika na matumizi ya kodi hizo? Ni kwanini kuna malalamiko?

Mathalani, masoko mengi Tanzania yanalalamikiwa kuwa wafanyabiashara wanatozwa ushuru kila siku kuanzia Shilingi 500 hadi maelfu  lakini sokoni hakuna vyoo, hata kama vipo ni duni na vibovu, maji ya kunywa na  miundombinu ya masoko ni chakavu.Mfano Soko la Mabibo Dar es Salaam, halifikiki nyakati za mvua.

Magari kwenye vituo vya mabasi yanalalamikia kutozwa ushuru kila siku lakini stendi hazina huduma bora kama vyoo, maji ya kunywa wala unafuu wa huduma. Zina mashimo na wahusika hawajali.

Kadhalika kwenye minada ya mifugo ushuru unachukuliwa kila siku tena mara kwa mara lakini hakuna maendeleo,  pengine hakuna hata choo, huduma ya chakula , maji ya kunywa na maeneo bora ya kuosha na kulaza au kuhudumia mifugo yote haya yanaelekeza wanaokusanya ushuru na kodi kutafakari njia zao.

Viongozi watambue kuwa kanuni  za kuchukua  kodi zinapaswa kuzingatia uwezo wa walipa kodi, lakini pia kodi hiyo  inakubalika kwa sababu mfumo wa kodi wenye haki ni lazima jamii na raia waone matunda ya kodi zao na siyo kuona wachache wakineemeka na wengine wakiwa fukara licha ya kulipa kodi na ushuru.

Hata hivyo, suala la migomo ya  kodi lisichukuliwe kwa wepesi kwani  maandamano ya kimkakati yanayoleta ghasia, uharibifu wa mali hata kuchoma bunge na kubeba majeneza na vitisho  ni hatari kwa  uwekezaji na shughuli za kiuchumi.

Hatari hizo za kisiasa zinaweka mazingira magumu kibiashara na uwekezaji na kukimbiza wawekezaji wa kigeni.
Kinachoonekana kinaweza kuchukuliwa kuwa ni cha nchi moja lakini ukweli ni kwamba picha ya kutisha inasaambaa Afrika nzima na kuongeza uwezekano wa bara hili kuogopwa na wawekezaji.

Ni  hatari zinazotishia  wawekezaji, mashirika na serikali kwa sababu matukio kama hayo yataathiri watu wengi na mipango ya kiuchumi  inayotarajiwa na hatua zilizofikiwa.

Kwa maneno rahisi, hatari ya migomo  ya kodi, maandamano na uharibifu wa mali yanatishia hatima za kisiasa na kuongeza  uwezekano kwamba biashara zinaweza kuharibiwa kwa sababu ya kukosekana kwa utulivu.

Migogoro na machafuko, mabadiliko ya fikra za vijana,  sera za kitaifa au mahusiano kati ya nchi,  sheria za biashara au kanuni za uwekezaji na masuala ya kulalamikia kodi ni mambo yanayotishia hatima ya  uwanja mzima wa uwekezaji na biashara.

CHAKUJIFUNZA

Ni vyema serikali ziwe na busara wakati wa kupanga namna ya kupata  kodi. Sera za ushuru lazima ziwe wazi na zinazokubalika na kueleweka kwa wananchi. 
Uwazi unaamanisha kuwa kutoza ushuru kwenye  vyakula na kutoa msamaha wa kodi kwa magari mapya kutoka kiwandani huko ughaibuni   ni jambo linaloweza kuonyesha kuwa serikali inayofanya hivyo haiwajali wananchi wake.

Serikali lazima itoe maeleza ya kutosha kwa wananchi kuhusu uhalali wa kutoza kodi na wanasiasa na uongozi wa umma waonyeshe kwa mfano kutumia kodi kwa kuleta  maendeleo ya taifa na siyo kuendeleza  ubadhirifu katika matumizi ya pesa ambazo wananchi wanataka zibadilishe maisha yao.

Serikali zikumbuke kuwa kundi kubwa ya raia ni vijana na wana nguvu na kuna haja kuwasaidia wawe na maisha bora ili kuwa na  utulivu wa kisiasa na kijamii na kwa ujumla kuwe na uongozi bora ili kuwe na amani.

Mataifa yanahitaji kuwa na umakini kwenye ushuru na uongozi bora kwenye masuala ya matumizi ya fedha. Kadhalika kuangalia na kufanya tafiti za mara kwa mara vipi kodi zinazotozwa zinawaumizaje wananchi?

Wafanyakazi na wafanyabiashara wanalalamikia  kodi ya ongezeko la thamani  VAT au kodi ya mshahara PAYE serikali ziangalie na kuchambua  mwelekeo wa kodi hizo  na athari kwa wahusika  kuepusha maandamano na kususa kufanyabiashara.