Licha ya TLP kujitutumua kuchagua M/Taifa, Ofisi ya Msajili haimtambui

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:19 PM Jul 03 2024
news
Picha: Mtandao
Mwenyekiti mpya Aivan Maganza.

BAADA ya mvutano wa miaka miwili, hatimaye Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), kimefanya uchaguzi wa Mwenyekiti Taifa, ambaye ni Aivan Maganza.

Hata hivyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imetangaza kuwa  haimtambui na uchaguzi huo haina taarifa zake.

 Akichaguliwa kwa kura 35  Jumamosi iliyopita kwenye  mkutano mkuu uliofanyika Dar es Salaam, anewashinda wagombea wengine Kinanzaro Mwanga na Stanley Ndamugoba waliovuna kura 10 kila mmoja, Richard Lyimo na Abuu Changaa walioambulia patupu,  ni kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi  Dominatha Rwechungura. 

Wakati Donatha, akisema hayo, ushindi wa Mwenyekiti  Maganza, hautambuliwi na  Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,  kwa maelezo kwamba haikuarifiwa wala kualikwa na kwamba taarifa zilizopo katika ofisi hiyo ni za  uchaguzi uliahirishwa.  

Wakati viongozi hao wakisema wanaye kiongozi mkuu wa chama,  Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, anasema ofisi yake haitambui uchaguzi huo, na haina taarifa zake.
 
 Anasema, kwa kawaida chama kinapofanya uchaguzi, ni lazima ofisi yake ipewe taarifa ya maandishi ili viongozi wake wawepo katika uchaguzi huo na kwamba haina barua wala chochote kuhusu mchakato huo.

 "Taarifa iliopo ofisini ni kwamba uchaguzi umeahirishwa, sasa huo umefanyikaje wakati kuna taarifa ya kuahirishwa? Mbona ofisi haina barua ya kufanyika kwa uchaguzi huo? Anahoji Nyahoza.
 
 Anafafanua kuwa ofisi inawasiliana na katibu mkuu wa chama kupata taarifa zote, na kwamba ilipokea barua kutoka kwa katibu mkuu ambaye ni Richard Lyimo ikielezea kuahirishwa kwa uchaguzi huo.
 
 "Juni 29 tulikuwa tunasimamia uchaguzi wa viongozi wa Chama cha ADC kwa sababu walileta barua rasmi inayoelezea kuhusu uchaguzi wao nasi tukaenda kuusimakia, lakini huo wa TLP hatuutambui," anasema.
 
 MAELEZO TLP
 Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi Dominatha Rwechungura wajumbe waliokuwapo katika uchaguzi walikuwa ni 55 Maganza  akaibuka mshindi hivyo wakawa wamechagua mwenyekiti mpya wa TLP taifa.

 Dominatha anasema, wamepata wakati mgumu kuandaa uchaguzi huo baada ya kuandika barua mara kwa mara kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ni mlezi wa vyama.
 
 "Lakini bahati nzuri tumefanikiwa kuitisha uchaguzi na sasa ninaomba  wajumbe tushikamane kujenga chama chetu ambacho marehemu Mwenyekiti Augustine Mrema alikipigania kwa nguvu zake zote," anawakumbusha.
 
 Anasema, uchaguzi huo ulifanyika nchini chini ya ulinzi  wa jeshi la polisi, kwa kuwa awali uliingia dosari kwa maelezo kuwa kulikuwa na viashiria vya kufanya hujuma za kuelekea kulazimishwa kuuahirisha tena.
 
 Katibu Mwenezi wa chama hicho, Geofray Laizar, anasema, ni wakati wa sasa wa kushikamana na kuachana na makundi kwa pamoja pasipo kuangalia dini wala kabila na kuondokana na makundi katika chama hicho.
 
 "Baada ya kumpata mwenyekiti mpya, sasa tutaunda safu ya ushindi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa kisha kumsimamisha mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025," anasema Laizar.
 
    FIGISI ZA UCHAGUZI
 
 Tangu kutokea kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa, Augustine Mrema ambaye alifariki Agosti mwaka 2022, kumekuwa na danadana za kumpata mrithi wake katika nafasi hiyo.
 
 Baada ya kifo hicho, Septemba mwaka huo, sekreterieti ya chama ilimchagua Hamad Mukadamu kuwa kaimu mwenyekiti ili baadaye ufanyike uchaguzi wa kumpata mwenyekiti taifa.
 
 Hata hivyo, tangu wakati huo, uchaguzi umekuwa ukipangwa na kuahirishwa mara kwa mara hadi Juni 29 ulipofanyika, lakini umekataliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutokana na sababu ambazo zimeelezwa na Nyahoza.
 
 Mara ya kwanza, chama kilipanga kufanya uchaguzi Januari 8 mwaka jana, lakini ukaahirishwa hadi Machi 6 2023, ukaendelea kupigwa dana dana  hadi Mei mosi mwaka huo huo na ukakwama.
 
 Baada ya hapo, ukapangwa kufanyika Desemba 28 mwaka jana, lakini haukufanyika, kisha ukapangwa kufanyika Januari 28 mwaka huu, ukaendelea kukapigwa kalenda hadi mwishoni mwa mwezi uliopita.
 
 Awali kabla ya Juni 29,Katibu Mkuu Lyimo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kuahirisha uchaguzi huo, kwa maelezo kuwa chama hakina fedha za kufanikisha uchaguzi huo.
 
 Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na upande unaomuunga mkono makamu mwenyekiti na kusema hizo ni figisi huku ukieleza kuwa wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wanajilipia gharama zote.
 
 Baada ya mvutano huo, upande huo wa makamu mwenyekiti ukaendelea na maandalizi ya uchaguzi huo uliofanyika Juni 29, lakini Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa I hauutambui.
 
 Wakati makamu mwenyekiti anaandaa uchaguzi, hatimaye ukafanyika, katibu mkuu aliandika barua kwenda Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayoelezea kuahirishwa kwa uchaguzi huo.
 
 Kwa mujibu wa Nyahoza, barua inayoelezea kuahirishwa kwa uchaguzi huo ambayo iliandikwa na katibu mkuu ndiyo inayotambuliwa, kwa kuwa amefuata utaratibu unaotakiwa wa kutoa taarifa kwa maandishi.