KUPUKUTIKA nywele si jambo jema, wala la kupuuza. Usifurahie kipara kuna tatizo.
Makala ya BBC Swahili inasema chakula unachokula ni muhimu katika kuufanya mwili kuwa na afya njema na kiakili pia, wakati hayo yakitokea mlo huo huathiri kila kitu kuanzia nywele, mifupa na ngozi pia.
Kunyonyoka nywele sio jambo dogo, kadhalika kuona zinapotea isivyo kawaida ni ishara ya kwanza kwamba kuna tatizo na mtu hapaswi kupuuza.
Kupururuka nywele kunaweza kusababishwa na mambo kadhaa kama msongo wa mawazo, pengine kuna uhusiano na vinasaba, mabadiliko ya homoni au matumizi ya dawa au tiba ya maradhi fulani.
Baadhi ya vyakula vyenye protini nyingi kama mayai na dengu, vitamini B kama mayai, maparachichi, madini ya chuma na zinki hasa nyama na njegere ni muhimu kuwa na nywele zenye afya.
Aidha, ikumbukwe kuwa mpangilio mbaya wa mlo kuwa na uzito mdogo na kula kupita kiasi, yanahusishwa sana na kunyonyoka nywele.
Huenda isijulikane hasa ni mambo gani maalum ya lishe husababisha kunyonyoka nywele lakini ukweli ni kwamba chakula ni kila kitu.
Lakini, kwa mfano, vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta kwa wingi si tu husababisha ugonjwa wa moyo, lakini pia matatizo na kuvimba seli.
Kwa haya miili hupokea mabadiliko na kukumbwa na kadhia ikiwamo kunyonyoka kwa nywele.
Bado haijafahamika rasmi ni chakula gani hasa kinachosababisha kunyonyoka nywele, lakini kwa mfano milo iliyojaa mafuta na sukari tele inatajwa kuudhoofisha mwili ni wazi hata nywele haziwezi kubaki salama.
Vyakula vilivyo na lishe inayozuia tatizo hili kama samaki na mafuta ya mbegu vinapaswa kupewa kipaumbele, baadhi ya mitazamo hushauri kuepuka vyakula vinavyosababisha kiungulia kwani vinaweza kutishia afya ya nywele, tafiti nyingi zinaunga mkono hilo.
Kwa mfano, wengine husema kwamba kufuata mlo wenye matunda mengi, mboga, nafaka, njugu, mbegu na mafuta asilia, ambayo yana sifa nyingi za kuzuia kiungulia, inaweza kusaidia kudumisha afya ya nywele.
VISABABISHI
Msongo wa mawazo umekuwa wa kawaida katika maisha ya kila siku. Ikiwa hali hizi za msongo zinaendelea kwa muda mrefu, tatizo la kunyonyoka kwa nywele huanza. Homoni ya Cortisol inayozalishwa na tezi ya ‘adrenal’ inahusiana na kupoteza nywele.
Msongo unapopungua, viwango vya homoni hii katika mwili vitarudi kwa kawaida. Lakini swali linabaki, inawezekana kudhibiti uzalishaji wa homoni hii kwa kutumia chakula? Jibu ni inawezekana.
Homoni ya Cortisol inaweza kuzuiwa kwa kujumuisha maparachichi, samaki wenye mafuta mengi kama sangara, mbegu, vyakula vilivyo na omega-3 fatty acids, vitamini na madini mbalimbali.
Vyakula vilivyochachushwa vimethibitishwa kuwa vyema katika kudhibiti upotevu wa nywele.
Hapa ndipo jukumu la ‘’gut microbiota’’ au matrilioni ya bakteria waishio ndani ya utumbo ambao ni muhimu.
Microbiota ni vijidudu ambavyo vinaishi katika mfumo wa kusaga chakula na mara nyingi ni muhimu mno, wanahusika katika afya na magonjwa huingiliana na virutubisho vinavyotumiwa, katika miili ambavyo hutofautiana kulingana na chakula watu wanachokula.
Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na urutubishaji wa lishe katika miili hutegemea idadi ya microbiota, idadi yao, ishara mbalimbali za kemikali na kimmeng’enyo wa chakula hutolewa katika mwili, husaidia pia kukabiliana na msongo wa mawazo.
Ikiwa lishe ni tofauti, ndivyo ilivyo hata bakteria kwenye utumbo.
Kwa hivyo kutumia vitu kama mtindi pamoja na vyakula vingine vilivyochachushwa vinaweza kusaidia kuimarisha afya ya nywele.
Kwa kufuata maelekezo hayo nywele zitakuwa na afya, kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha San Jorge Sayansi ya Afya PDI Kitivo Pilar Argento Arizona.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED