Majiko ya gesi 3,255 kutolewa kwa bei ya ruzuku Longido

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:16 PM Dec 04 2024



Mbunge wa Longido na Naibu Waziri wa Madini,Dk. Steven Kiruswa akimkabidhi jiko la gesi Nanyori Laizer mkazi wa Kata ya Ngarenaibo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mbunge wa Longido na Naibu Waziri wa Madini,Dk. Steven Kiruswa akimkabidhi jiko la gesi Nanyori Laizer mkazi wa Kata ya Ngarenaibo.

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza usambazaji wa majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku Wilayani Longido Mkoani Arusha ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034.

Hayo yameelezwa jana Desemba 03, 2024 wilayani Longido na Mhandisi wa Miradi wa REA, Kelvin Tarimo wakati wa mkutano wa Mbunge wa Longido na Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa wa kuelezea utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya serikali wilayani humo.

"Tupo hapa Wilayani Longido kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na kuanza rasmi uratibu wa mradi wa kusambaza na kuuza majiko ya gesi (LPG) ya kilo 6 ambapo kwa Wilaya ya Longido pekee jumla ya majiko 3,255 yatauzwa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50," alisema Mhandisi Tarimo.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi, Kiruswa aliipongeza REA kwa kutekeleza miradi yake kwa ufanisi ambapo alisema kwa wilaya hiyo ya Longido hadi sasa vijiji vyote 51 vimefikishiwa umeme na kazi inaendelea ya kuunganisha vitongoji.

Mhandisi wa Miradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Kelvin Tarimo (mwenye fulana nyeusi) akitoa elimu ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wananchi wa Longido wakati zoezi la kuanza rasmi kusambaza majiko ya gesi (LPG) kwa bei ya ruzuku ya 50% wilayani humo.

Mhandisi Tarimo alisema Wakala wa Nishati Vijijini unalo jukumu la kuhakikisha Watanzania wanaachana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama kama ambavyo imeelekezwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Aidha, alitoa rai kwa wananchi kutumia umeme kujiletea maendeleo hasa ikizingatiwa kuwa umeme ni fursa.

"Wakala unatoa rai kwa wananchi kutumia umeme kujiletea maendeleo ya kiuchumi na pia kupikia kwani umeme ni moja kati ya nishati rafiki kwa matumizi ya kupikia," alisisitiza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa Longido alipongeza jitihada za Serikali za kuwasambazia nishati safi ya kupikia mbayo wamesema ni hatua nzuri ya kulinda afya zao na mazingira kwa ujumla.

Mhandisi wa Miradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Kelvin Tarimo akihamasisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia kwa wananchi wa wilaya ya Longido (hawapo pichani) wakati wa kuanza kwa utekelezaji wa kusambaza majiko ya gesi (LPG) yanayotolewa kwa bei ya ruzuku wilayani humo.

Sinyati Yohana mkazi wa Kata ya Ketumbeine amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea kero wananchi wa Longido hususan wanawake na watoto ya kutembea umbali mrefu kusaka kuni kwa ajili ya kupikia.

Naye Larasha Lulungen mkazi wa Kata ya Matale alisema uwepo wa nishati safi ya kupikia wilayani hapo ni hatua ya kupongezwa kwani inakwenda kuimarisha afya za wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia kuni kupikia.

"Tulikuwa tunasikia tuu nishati safi lakini leo tumeelimishwa na pia tumeshuhudia majiko ya gesi yaliyotolewa na Serikali kwa ruzuku," amesema Lulungen.

Wakala wa Nishati Vijijini unaendelea kutekeleza mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wameachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama.

Mbunge wa Jimbo la Longido na Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa (wa pili kushoto) akiwa na wananchi wa Longido wakati wa kuanza usambazaji wa majiko ya gesi wilayani humo yaliyotolewa kwa bei ya ruzuku ya 50% ikiwa ni jitihada za Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.