Wanufaika wenye ulemavu TASAF waishukuru Serikali

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 01:57 PM Dec 04 2024
Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF akiongea na mlengwa katika banda la TASAF katika kuadhimisha siku ya watu wenye Ulemavu duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa diamond jubilee Jijini Dar es Salaam
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF akiongea na mlengwa katika banda la TASAF katika kuadhimisha siku ya watu wenye Ulemavu duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa diamond jubilee Jijini Dar es Salaam

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Walemavu, wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao ni walemavu wameiomba Serikali kuendelea kuwasaidia huku wakikiri kuwa mfuko huo umewabadilisha maisha.

Wanufaika hao wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuuongezea uwezo mfuko huo ili kuwafikia watu wengi zaidi wenye uhitaji. Akizungumza Kibaha, Pwani, mmoja wa wanufaika hao, Amina Mrupe, alisema awali walikuwa wakikabiliana na changamoto kubwa, lakini ruzuku ya TASAF imeleta mabadiliko makubwa kwao.

"Tunamuomba Rais Samia aiongezee nguvu TASAF ili iwafikie walemavu wengi zaidi. Tuna uhitaji mkubwa kutokana na hali zetu, hivyo tunaiomba Serikali iendelee kutusaidia," alisema Amina.

Alifafanua kuwa kupitia TASAF ameweza kuanzisha biashara mbalimbali kama kuuza karanga, kutengeneza batiki, viungo vya chai, chakula, na sabuni. Biashara hizo zimemwezesha kupata kipato na kujikimu kimaisha.

"Awali nilikuwa napokea ruzuku ya Sh. 30,000 kila mwezi, baadaye ikapanda hadi Sh. 12,000 kwa kuwa sasa naishi na mume wangu tu. Pia nilipata mtaji wa Sh. 500,000 kutoka TASAF, ambao ulinisaidia kuanzisha biashara ya batiki na kuuza karanga mbichi na za kukaanga," alisema.

Aliongeza kuwa maisha yake yamebadilika sana, tofauti na awali, ambapo sasa anaweza kugharamia mahitaji muhimu kwa familia yake. Alisisitiza umuhimu wa Serikali kuangalia kwa karibu mahitaji ya walemavu na kuongeza nguvu TASAF kwa kuwa imekuwa msaada mkubwa kwao.

Mnufaika mwingine, Nuru Ally mkazi wa Kigogo, Dar es Salaam, ambaye ni mlemavu wa kutoona, alisema ameondolewa kwenye orodha ya wanufaika wa TASAF baada ya hali yake ya kiuchumi kuimarika. Kupitia TASAF, amejifunza kutengeneza viungo vya chai, viungo vya chakula, na sabuni za chooni, biashara ambazo zimekuwa chanzo cha kipato chake na zimemwezesha kuhudumia familia yake yenye watoto wanne.

"Awali walemavu walionekana kama ombaomba, lakini kupitia TASAF nimeweza kujitegemea kiuchumi. Sasa hivi naendesha maisha yangu kwa heshima," alisema Nuru.

Hata hivyo, wanufaika hao walieleza changamoto ya ukosefu wa soko la bidhaa wanazozalisha. Wameiomba Serikali kushughulikia suala hilo ili kuongeza ufanisi na tija kwa walemavu wanaojitahidi kujitegemea.

Maadhimisho ya Siku ya Walemavu Duniani yanaendelea kusisitiza umuhimu wa kuwajengea mazingira bora na jumuishi watu wenye ulemavu ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.