Unayedaiwa HESLB ‘fichuka’ kampeni fichua inaanzia kwako

By Reubeni Lumbagala , Nipashe
Published at 12:20 PM Jul 09 2024
Wahitimu wanapofurahia mahafali wakumbuke kurejesha mikopo ya bodi.
PICHA: MTANDAO
Wahitimu wanapofurahia mahafali wakumbuke kurejesha mikopo ya bodi.

ELIMU ni nyenzo ya kumwezesha mtu kumudu na kutawala mazingira ambayo ndiyo maisha yake. Ni wazi unapopata maarifa, stadi na ujuzi ni msaada wa kujua namna ya kuendesha maisha kwa kuwa yale uliyojifunza unayatumia kusongambele.

Kimsingi, elimu ni ghali, ni gharama, ndiyo maana kuendesha na kutoa elimu, serikali, asasi za kiraia, mashirika, mataifa washirika wa maendeleo na wananchi wamekuwa bega kwa bega kuchangia maendeleo ya elimu.

Wanatoa fedha, kugharamia mafunzo ya walimu, sare, kujenga miundombinu, vifaa vya ujenzi, na vya wanafunzi, kompyuta, samani na vifaa vya michezo ili kuwezesha elimu kuwafikia wanafunzi popote katika mazingira bora yanayochochea uelewa.

Serikali mdau namba moja wa kila kitu anawapa mikopo wanafunzi wa vyuo vya kati  na vikuu ili kumudu gharama za elimu ya juu kuanzia  kujikimu,  ada, chakula, malazi, vitabu na mafunzo kwa vitendo .

Ili kuratibu kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo, ipo Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), iliyoundwa tangu 2004, ikihusika na kupokea maombi, kuyachakata na mwisho kutoa orodha ta waliokidhi vigezo vya kupata mikopo.

Kwa wale waliokidhi kupata mikopo, wanapata taarifa za kiwango au asilimia za mikopo walizopata ili kujua gharama nyingine wanazopaswa kuchangia na kuzisaka kabla ya kuingia vyuoni.

 Mathalani, mwanafunzi aliyepata mkopo wa asilimia 80 na ada ya kozi yake ya chuo kikuu ni Shilingi 1,000,000 kwa mwaka, bodi ya mikopo itampatia mnufaika Sh.800,000 naye ataongezea 200,000 kukamilisha ada kwa mwaka.

Ikumbukwe kuwa HESLB haitoi msaada wa fedha bali inakopesha wanafunzi kwa mkataba kuwa atakapohitimu, arejeshe mkopo uliotumika kumsomesha ili pesa hizo zitumike kusomesha wengine sasa na miaka ijayo. 

Kwahiyo, kila mnufaika wa mkopo, anapaswa kuurejesha baada ya kuhitimu akiajiriwa au kujiajiri.

 Kwa walioajiriwa katika sekta binafsi au ya umma wanapaswa kurejesha asilimia 15 ya mshahara wao wa kila mwezi na kwa wale waliojiajiri wanayo fursa ya kuwasiliana na HESLB na kuweka utaratibu wa kiwango cha fedha wanachoweza kurejesha kila mwezi kulingana na vipato.

Ili kuongeza wigo wa marejesho ya fedha kutoka kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu, HESLB imekuja na kampeni “fichua kuwa hero wa madogo” ili kuwamulika na kuwafichua wanufaika walio na ajira lakini hawarejeshi fedha zilizowasomesha.

Kampeni hii maalum ya kuwasaka wadaiwa sugu 50,000 ili kukusanya Sh.bilioni 200.

Fichua inayozinduliwa rasmi Juni 28, 2024 na itaendeshwa kwa miezi miwili ikilenga kuongeza makusanyo ya mikopo kw kuwafichua wanufaika ambao licha ya kuwa na ajira haleti rejesho HESLB.

Mkurugenzi wa HESLB Dk. Bill Kiwia, akizindua Fichua anasema:“Kampeni hii inalenga kuwashirikisha wananchi kutimiza jukumu la kizalendo la kuwafichua wadaiwa wenye kipato lakini hawajitokezi kurejesha mikopo.”

Wanufaika wawe wazalendo kwa kutambua kuwa fedha zilizotumika kuwasomesha ni za Watanzania ambao walikubali wapewe ili wasome.

Lakini pia ni rejesho la mikopo hiyo kutoka kwa waliowatangulia zilizokusanywa zikapatikana nao wana wajibu wa kuzirudisha 

Hivyo basi, wajue wana deni warejeshe fedha hizo hata kama bado hawajaanza kukatwa moja kwa moja kupitia mishahara au ajira binafsi.

Dk. Kiwia anawataka wananchi kuwafichua wadaiwa sugu wa mikopo ili kuwezesha wanufaika wengi zaidi kunufaika na mikopo ya elimu ya juu. 

“Ili kutoa taarifa za wadaiwa, mwananchi anapaswa kutuma jina la mnufaika, chuo alichosoma, eneo analofanyia kazi iwe kampuni, kiwanda au asasi, shule kama amejiajiri au kuajiriwa na eneo ilipo taasisi hiyo,” anasisitiza Dk. Kiwia. 

Wananchi waiunge mkono HESLB kwa kuwafichua wadaiwa sugu ili kuongeza makusanyo ili Watanzania wengi zaidi wapate fursa ya kufikia elimu ya juu.

JIFICHUE MWENYEWE

Pamoja na kwamba HESLB imeanzisha kampeni hiyo, ni vyema mnufaika yeye mwenyewe akajifichua kwa kuwasiliana na bodi moja kwa moja ili kuweka utaratibu wa kulipa mkopo wake kupitia namba maalum ya malipo (control number) hasa waliojiajiri wenyewe. 

Kujifichua ni uzalendo kwa kuzingatia kuwa waombaji wengi wa mikopo wanatoka familia maskini ambazo haziwezi kumudu gharama za chuo, kwahiyo kujitokeza ni kutambua umuhimu wa kuwezesha wengine kusoma hasa wanaotoka familia maskini.

WAAJIRI WAFICHUENI 

Waajiri ni wadau muhimu katika kurejesha mikopo wanufaika hao wanapopata kazi katika ofisi zao. Kwa upande wa waajiri wa serikali, imekuwa rahisi kuwapata kutokana na mifumo iliyopo sasa na ndiyo maana mwajiriwa mpya wa sekta ya umma anapoanza kazi kama alipata mkopo, anaanza kulipa deni kupitia mshahara wake wa kwanza au wa pili anapoanza kazi.

Changamoto ipo kwa baadhi ya waajiri wa sekta binafsi ambao baadhi yao wamekuwa wakificha au kuchelewa kutuma taarifa za wafanyakazi wao ambao baadhi yao ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Kwahiyo, kupitia kampeni ya fichua, waajiri wote wa sekta binafsi na umma watoe taarifa sahihi za waajiriwa wao ili serikali kupitia HESLB iweze kukusanya fedha zaidi ili vijana wengi wagharamiwe elimu ya juu.

Muhimu zaidi ni kwa wanufaika wenyewe kujifichua kabla ya kufichuliwa wakumbuke kulipa mkopo si mpaka uwe umeajiriwa serikalini au katika sekta binafsi.

Unaweza kuanza kulipa kidogo kidogo hata kupitia ajira binafsi uliyonayo, mathalani,  kwenye kilimo, ufugaji, bodaboda, mamalishe, fundi simu, ususi na  ujenzi.

Ikumbukwe kuwa kampeni ya Fichua ni maalum kwa wanufaika ambao wameshahitimu masomo yao na wana kazi za kuwaingizia kipato lakini bado hawajaanza kulipa mikopo hiyo. “Lengo ni kufichua wadaiwa sugu ambao wana vipato, lakini wako mitaani wanaendelea na shughuli zao na hawashtuki kulipa madeni.,” anakumbusha Dk. Kiwia. 

Mwandishi ni mwalimu Sekondari ya  Mlali iliyoko Dodoma. M

Maoni: 0620 800 462.