TEKNOLOJIA: Kinu na mtwangio teknolojia ya karne nyingi zaidi duniani

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 12:12 PM Jul 09 2024
news
PICHA: MTANDAO
Kutwanga kwenye kinu hakuna umri hata watoto wanaweza.

KAZI ya kuandaa nafaka au vitu vingine vinavyokobolewa, kusagwa na kupondwa ili kupata unga na bidhaa nyingine leo hufanywa kwa kutumia mashine za kisasa.

Ukiingia jikoni zipo mashine, mfano, blenda zikisaga matunda kupata juisi, hutengeneza mtori, hutumiwa kusaga nyanya na kuchanganya vyakula vya watoto. Pia, hata nazi hukunwa kwenye mashine zinazotumia umeme.

Lakini, lazima pembeni kuna kinu kinachotumiwa kuponda kisamvu, kutwanga viungo, karanga, kweme, dawa na wakati mwingine kupwaga nafaka ambazo mashine huenda haziwezi kazi hiyo.

Kinu na mchi ni zana za siku nyingi na inayoendelea kutumiwa  na kwa kutazama kazi zake , teknolojia ya kuponda na kusaga vyakula imeboreshwa zaidi.

Kwa Tanzania karne nyingi na karibuni kabla ya Uhuru 1961 matumizi ya mashine kusaga nafaka, kuzikoboa au kupwaga hayakuwepo, karibu nchi nzima kilitumika kinu na mtwangio. Baadhi ya jamii ziliongeza pia jiwe la kusagia ili kuponda au kutwanga nafaka.

Nafaka kama mahindi, mchele, mtama, uwele na ulezi vilipitia mchakato huo, lakini leo kazi hiyo imerahisishwa kwa kutumia mitambo inayoendeshwa kwa umeme, dizeli au petroli kusaga, kukoboa na kushughulikia nafaka hizo.

Kinu ndicho kinachokoboa, kuponda, kupwaga na , kutwanga nafaka kama mahindi, mtama, mchele na uwele ili kujipatia unga uwe wa ugali, chapatti, uji, mikate, vitumbua na nafaka za kupika kande.

Teknolojia hiyo ya kinu cha asili, inatumika hadi leo mijini na vijini mfano huponda kisamvu mijini na vijijini, wapo wanaokoboa mpunga, wengine hukoboa na kutwanga kahawa, kutwanga mlenda, dawa mbalimbali za binadamu na wanyama.

Kinu cha asili ya Tanzania kinatokana na mti gogo linakatwa na kutengeneza shimo katikati kutegemeana na ukubwa unaotakiwa. Vipo vyenye ujazo mdogo, vingine hufikia hata debe au ndoo nzima. Ili kutwanga unahitajika mtwangio ambao ni mti pia.

Kuna upande huwa mpana au mkubwa zaidi na mwingine mwembamba lengo ni kuuwezesha ufae kwenye matumizi mbalimbali kuanzia kuponda a hadi kupwaga hasa mahindi au mtama.

Kinu kinaweza kuwa na mitwangio mbalimbali hata mitano.

Kinu kinatumiwa kuondoa maganda ya nje ya nafaka hasa mahindi, mtama, mpunga na uwele wakati mwingine maji hutumika kulowanisha hasa mahindi, japo mpunga hayatumiki.

Kinu ni teknolojia inayoendelea kutumiwa hata leo ndiyo maana utakikuta mijini na vijijini. Hakuna jiko lisilokuwa na kinu japo kidogo ili kutwangwa viungo mbalimbali vya pilau na vingine vya kuunga vyakula.

Kinatumika kutwanga mboga mfano mlenda, kisamvu, kadhalika dawa za aina mbalimbali zinazotumiwa mijini na vijijini. 

Makabila mbalimbali ya Tanzania yanakitumia kifaa hiki na yamekipa jina , mfano Kipare ni ‘kitwi na ‘mthi’, Wasukuma huita ‘litoli na mwisi’ wakati Kihaya huitwa ‘ekinu na emutwangilo.’ 

Historia ya kuponda mazao mbalimbali ili kuandaa chakula kwa karibu dunia nzima au jamii zote ziwe maskini au za matajiri ilianza kwa kutwanga ndipo ulikuwa mwanzo wa ujio wa kinu.

Kutwanga au kuponda nafaka ambazo ni chakula muhimu ili kupata nguvu kwa jamii nyingi, kulikuja na ugunduzi wa kinu na mtwangio hasa vya miti, japo kuna madai kuwa vipo vinu vya mawe ya granite hasa huku Asia.

Mchakato wa kuandaa vyakula ulihusisha pia kuwa na jiwe la kusagia, ambalo jamii zilikuwa nalo kuanzia zama za Masiha Yesu Kristo hata na Tanzania na Afrika nzima. Mfano Nigeria kuna jiwe hilo ambako kwa Wayoruba linaitwa olo.

Jiwe hili lilitumika nyumbani kusaga mahindi, mtama, ngano, mihogo kupata unga. 

Familia zilisaga mbegu kama karanga, korosho, mbegu za maboga, wakati mwingine hata dawa. Kwa ujumla ilikuwa kazi ngumu ndiyo maana kinu kilihitajika.

Watafiti wa akiolojia na anthropolojia wanaoangalia mienendo ya mambo ya kale wanaeleza kuwa kabla ya wanadamu kuwa na moto jiwe la kusaigia,kinu na mtwangio vilihusika na ndicho kiwanda cha chakula.

Ni chombo cha kwanza cha kutayarisha chakula, kinu kikitajwa kuwa ni cha zamani miaka mingi kabla ya ujio wa Kristo.

Inaelezwa kuwa chombo hicho kilitumika kwa ajili ya masuala ya kiroho kwenye jamii za Wahindi ili kuwaepusha na mapepo na magonjwa. 

Lakini pia kinaweza kuonekana kuwa kifaa hicho kina historia ya kutumiwa China, Misri na nchi nyingine za Afrika.

Kadhalika akiolojia inaonyesha jinsi kilivyotumiwa kuandaa nafaka za kupikwa kwenye sherehe za kidini za Warumi na hata Waamerika wa asili maarufu Red Indians.

Kuna ukweli kuwa kote duniani kwenye watu wa utamaduni mbalimbali walikuwa na jiwe la kusaga nafaka na baadaye kikafuata kinu na mtwangio kuandaa vyakula vyanafaka.

Kwa baadhi ya jamii kinu kilitumiwa vibaya kilikuwa kitanzi cha watoto waliokuwa hawatakiwa na jamii mfano wenye ulemavu, kwa mfano Wapare kabla ya Uhuru na ujio wa mafundisho ya dini, wanadaiwa  walijaza maji kwenye kinu na kuwatumbukiza watoto hao kichwa chini miguu juu ili kuwaua.

UMUHIMU

Ni kifaa kinachotumika maeneo mengi muhimu karibu dunia nzima. Kikiwa na sura tofauti hata leo kinatumika maabara za utafiti, jikoni, kwenye viwanda vya dawa na hata wanaotoa tiba za asili.

Kwa upande wa uchongaji kinu na mtwangio ni urembo huchongwa na wana sanaa za kuchonga vinyago, wapo wanaotumia ‘marble’ , soapstone,’ na mpingo lakini pia udongo wa mfinyanzi kuviunda.

Kwa ujumla kinu na mtwangio ni teknolojia inayoendelea kuishi na huenda itachukua karne nyingi kuondoka.