Taka plastiki sasa ni ‘baraka’ wenye bajaji, magari na boda

By Beatrice Philemon , Nipashe
Published at 12:22 PM Jul 09 2024
 Meneja Uzalishaji, Abdul Lwangisa, akielezea matumizi ya vipuri wanavyotengeneza  kwa taka za plastiki.
PICHA: DIT
Meneja Uzalishaji, Abdul Lwangisa, akielezea matumizi ya vipuri wanavyotengeneza kwa taka za plastiki.

KUNA msemo kuwa taka ni fursa tena ni pesa. Hili linadhihirishwa na kile kinachofanywa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ambayo kwa kurejeleza taka za plastiki, imeibua fursa kibao.

Mosi imewaletea vijana ajira, ambao wanafurahia kuuza plastiki na kujipatia mapato, taasisi inazalisha vipuri kupunguza kuagiza kutoka nje na kubwa zaidi DIT imefanikisha ulinzi na utunzaji wa mazingira, anasema Meneja Uzalishaji, Abdul Lwangisa.

Anaongeza kuwa DIT inarejeleza kwa kuchakata chupa na taka za plastiki kutengeneza vipuri vya magari, pikipiki, bajaji na mitambo mingine.

Anaeleza kuwa ni mafanikio yaliyopatikana baada ya kufanya utafiti na kuona kuwa taka za plastiki zipo nyingi mitaani na pia uhitaji wa vipuri vya mitambo, magari, pikipiki na bajaji ni mkubwa na haujapata majawabu.

Akizungumza na Nipashe katika Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Meneja Uzalishaji wa DIT, anasema waliamua kugeuza changamoto ya taka za plastiki kuwa fursa na kuongeza kipato kwa jamii na taifa.

“Wananchi wanaokusanya taka hizi na kuuza wanapata fedha, nasi tunapozalisha vipuri kama rubber boot ambayo ni mipira ya kuzuia tope na maji yasiingie kwenye beringi za tairi.

“Bush rabbers ambayo ni mipira ya kuzuia mikwaruzo ya chuma kwa chuma kwenye vyombo vya moto na corn rubber mipira inayowekwa kwenye matairi ya bajaji kuzuia tope na maji visiingie” anasema.”Lwangisa.

Anataja vipuri vingine kuwa ni ‘spring bushes, vifaa vinavyowekwa kuzuia msuguano kati ya vyuma na vyuma na vingine ni ‘hydraulic oil seal, escalator, elevator roller na chicken plucker’ kuwa vyote hupatikana.

Anasema pamoja na kuzalisha vipuri wameanzisha kiwanda cha kuchakata taka za plastiki ndani ya  taasisi hiyo iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Lwangisa anafafanua kuwa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha vipande 3,500 vya ‘corn rubber’ kwa ajili ya bajaji, spring bushes za magari 4,500 na vipande 4,000 vya suspension bushes vya pikipiki, vyote vikizalishwa kwa siku moja.

“ Kwa wananchi au wafanyabiashara wanaohitaji vipuri hivi vyote vimethibitishwa ubora na Shirika la Viwango (TBS ), bei zetu ni nafuu na bidhaa zinapatikana kwa urahisi,”anasema Lwangisa.

MAKUNDI WANUFAIKA

Meneja Uzalishaji , anasema wanapata taka za plastiki kutoka kwa vijana, wanawake na makundi ya wenye mahitaji maalumu, wakinunua tani mbili za taka kwa siku wakiwafuata wauzaji katika maeneo yao.

“Kilo moja inanunuliwa kwa Sh 300 au 450 kulingana na hali ya soko,” anasema Lwangisa

Mbali na hilo, pia teknolojia hiyo ilishindanishwa na vyuo 16 vya elimu vilivyo chini ya Wizara ya Elimu Tanzania Bara na Visiwani, kwenye Mashindano ya Sayansi na Teknolojia Kitaifa yaliyofanyika Dodoma mwaka 2019.

Anasema: “Teknolojia yetu ya kuchakata taka za plastiki ilichukua nafasi ya pili kwa ubunifu bora wa mashine na bidhaa zinazolenga kuwakomboa wananchi kiuchumi na kutunza mazingira.” 

Lwangisa anasifu juhudi hizo akisema teknolojia hiyo iko sokoni kusaidia wananchi wanaomiliki vyombo vya moto kupata vipuri kwa bei nafuu na pia vinavyodumu na vyenye ubora.

“Tunapatikana Dar es Saalam hapa DIT, kwa Dodoma tupo Majengo, Arusha- Ngarenaro, Songwe tunapatikana mtaa wa kwa Mpemba, wakati tuko Uyole kwa upande wa Mbeya Uyole na Mwanza ni kwenye kampasi ya DIT,” anasema Lwangisa.

Anasema vijana 30 wana ajira na wanaendesha maisha yao kutokana na mradi huo.

KUPATA TEKNOLOJIA

Meneja huyo anasema DIT inafundisha teknolojia hiyo kwa wanafunzi wake ili wakihitimu wafungue kampuni zao,kujiajiri, kuwa wajasiriamali na kuajiri wengine kuongeza kipato na kupunguza uharibifu wa mazingira.

“ Wapo wanafunzi watano katika taasisi yetu wanasoma kozi fupi ya kuchakata taka za plastiki na pia wapo wengine kutoka viwandani wanaofika DIT kujifunza,”anasema na kuongeza kuwa taasisi inapokea watu wenye elimu ya darasa la saba hadi ya vyuo vya elimu ya juu.

Mnufaika wa bidhaa hizo Domina Lwakatare kutoka Chanika Dar es Salaam, anapongeza teknolojia hiyo ya kuchakata taka za plastiki kwa sababu zimekuwa ni changamoto kubwa kitaifa.

Anasema watu wanazitupa hovyo zinaharibu mazingira, nyingine zimejaa mtoni, maziwani na baharini wakati wa mvua zinaziba mitaro mitaani na makazi yanakuwa machafu na mazingira kuchafuliwa.

Anasema kwenye maziwa na mito zinaathiri samaki na viumbe wengine na kuharibu mifumo yote ya ikolojia kama wataalamu wanavyosema.

Domina anasema ingawa taasisi hiyo imeanzisha mradi huo ,wananchi waelimishwe jinsi ya kukusanya taka na kuzihifadhi ikibidi DIT wapanue maeneo ya uzalishaji ili wawanufaishe wananchi mikoani.

Aidha, anasema kuelimisha wananchi mbinu na umuhimu wa urejelezaji taka ili kutunza mazingira uwe ajenda ya kudumu kwenye mikutano ya vijiji, mitaa na kwenye nyumba za ibada ili kufanikisha kampeni hiyo.