WIKI iliyopita shujaa Rose, anaelezea alivyowaingiza mabinti shuleni, mbinu alizotumia kufikia mafanikio na leo anabainisha alivyogombea uongozi kisiasa…
Rose Njiro (40) anasema katika kuonyesha kwamba mwanamke anaweza na kuweka msisitizo kwamba mila kandamizi walizokuwa wanazishikilia Wamaasai kumwona hafai, hawezi na ni laana, aliwaonyesha kuwa hawakuwa sahihi.
Anajitosa kugombea ubunge mwaka 2021 katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Ngorongoro baada ya mbunge aliyechaguliwa kufariki.
Anasema alikuwa mwanamke pekee kati ya wanaume 16 waliojitokeza kuomba ridhaa ya CCM, kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama.
“Nilitaka kuonyesha kuwa binadamu wote ni sawa na wana uwezo sawa, kwa sababu haijawahi kutokea mwanamke wa Kimaasai akagombea uongozi kwenye kitongoji au uongozi wa kimila. Walionekana ni laana kufanya hivyo, na hata historia ilikuwa inaonyesha kuwa tangu jimbo la Ngorongoro lianzishwe mwanamke hajawahi kugombea ubunge au kupatikana kiongozi wa kike iwe ni Mmasai au asiye wa jamii hiyo.”
“Ule uthubutu uliwafungulia njia wanawake wengine katika jamii yetu hasa kwenye vyama vya siasa huku kuna wengine wameanza kugombea na wamechaguliwa. Lakini ningepewa nafasi ingekuwa fursa nzuri kwangu kuitumia kutafuta majibu ya migogoro ya ardhi ambayo imedumu kwa miaka mingi.”
Anasema shida kubwa inayochangia hiyo ni kukosekana kwa mahusiano mazuri kati ya wananchi na serikali ndiyo maana haiishi, wakipatikana viongozi migogoro inazidi mpaka miaka mitano inaisha na hakuna maendeleo.
“Wilaya ya Ngorongoro kuna wawekezaji wengi, kuna fursa kubwa ya maendeleo, lakini kumekosekana mtu sahihi wa kuunganisha ili wananchi waachane na migogoro ya kila badala yake watumie fursa hizo kujiletea maendeleo,” anasema Rose.
Anasema katika kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka kesho, tayari ameunda vikundi vya kuelimisha wanawake namna ya kusimama kugombea.
“Na nimewaambia waitumie vizuri hii fursa ambayo kwa sasa jamii imeamini uwezo wa mwanamke, wajitokeze kwa wingi wagombee kwa sababu uwezo wetu wanawake umetambulika na jamii yetu,” anasema.
KUGOMBEA JIMBO
Rose anasema katika uchaguzi mkuu ujao amejipanga kugombea tena kwa mara ya pili katika jimbo la Ngorongoro akijinasibu kwamba kwa kazi ambazo amezifanya na kuonekana kwa jamii, ana uhakika wa kushinda kwa kishindo endapo chama chake cha CCM kitaridhia kumteua kuwania nafasi hiyo.
“Na sasa hivi napambana kwanza kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kuhakikisha kwenye nafasi hizo wanawake wengi wanaingia, kwa sababu ili nifanikiwe kule mbele lazima nihakikishe kwamba kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa tumefanya vizuri.
KUSAIDIA WATOTO
Mbali na taasisi hiyo, Rose anasema mwaka jana alianzisha pia kituo cha kusaidia watoto wa kike wanaopitia ukatili wa kijinsia ikiwamo wale wanaokimbia kuozeshwa kwenye umri mdogo.
“Kwa hiyo tumetengeneza sehemu salama ambayo wanaishi, kama wanaendelea na shule wanatokea hapahapa kituoni, na wakati huo huo tunaendelea kutengeneza mahusiano na familia zao japo mahitaji yote tunawapatia sisi kituoni, pamoja na mambo mengine, tunawafundisha ufundi wa kushona, lakini wapo wanaosoma shule za msingi, na sekondari.
MFANYAKAZI AZUNGUMZA
Mmoja wa wafanyakazi katika taasisi hiyo ya MWO, Saitoti Salingi, anasema Rose amefanya kazi ya kuleta mapinduzi katika maeneo mengi lakini kubwa ambayo imeleta matokeo mazuri na makubwa ni ya kufanya mapinduzi kwa jamii ya kimaasai kutoka kuamini mtoto wa kike ni laana hadi kufikia kuamini kwamba anaweza na kukubali kumpa nafasi ya uongozi katika jamii yao na kumruhusu kwenda kugombea kwenye chaguzi za kitaifa.
“Wakati anaanza kupambania hili, kila mmoja alimuona kama amechanganyikiwa wakisema tangu enzi za mababu na historia nzima ya jamii ya kimaasai haijawahi kutokea mwanamke akawa kiongozi sasa yeye anatawezaje, akapigwa vita kubwa si tu na viongozi wa mila kutoka ndani ya jamii yake lakini hata wale ambao wana nafasi za kisiasa kama madiwani, wenyeviti wa vijiji, lakini kwa Rose haikumyumbisha aliendelea mbele hadi alipohakikisha amevunja huo mwiko.
“Kuna wakati hata sisi tulikuwa tunaogopa na tunamshauri kwamba aachane nao tu maana ilikuwa ni hatari kwake, usalama ulikuwa ni mdogo lakini hakutusikiliza na baadae tulikuja kumwelewa nini alikuwa anaona mbele baada ya kuona haya mafanikio yaliopo kwa sasa katika jamii hii,” anasema Salingi.
HISIA ZA MTOTO WAKE
Kiranda Saning`o ni mtoto wa Rose, anasema wao wanafurahia kazi anayofanya mama yao licha ya kupitia misukosuko mingi lakini wanamuunga mkono.
“Tumeshuhudia maisha aliyopitia mama yetu wakati tunakua na mpaka sasa tumefikia hapa, ukweli kama una roho ndogo unaweza usikubaliane naye lakini sisi tunamuunga mkono kwa sababu akiacha yeye kufanya hakuna atakayefanya na wanawake wataendelea kuteseka katika jamii ya kimaasai,” anasema Kiranda.
“Tunachoshukuru ni kwamba mama anasali sana na sisi tunamuombea, tunaamini Mungu anamlinda hakuna wa kumdhuru. Na kutokana na moyo wake huo wa kupambania watu wengine, ametuambukiza na sisi tunafanya hivyo, mfano mimi nikisikia kuna mtu yeyote ananyanyaswa hata ni shuleni huwa ni lazima nikaripoti na wakati mwingine namshirikisha mama.”
SAUTI YA DADAKE
Dada yake Rose, aliyejitambulisha kwa jina la Nayo Laang, anasema wakati ndugu yao huyo anapambania ukombozi wa mwanamke katika jamii hiyo, ilifika wakati wakawa wanatamani asiende tena kijijini kwao, kwa sababu wazee walikuwa wametangaza kwamba akionekana tu wanamuua kwa sababu anafundisha tabia mbaya wanawake.
“Siku moja alipofika kijijini, mwenyekiti wa kijiji aliita watu wakakusanyika, halafu akawa ameshika sime, tukamuonyesha Rose ishara kwamba akimbie wanataka kumuua, lakini yeye alikataa, sasa wakati ndio Mwenyekiti anatoa sime ili ampige nayo, mimi nikakimbia kwenda kumkumbatia na hapohapo baadhi ya wanawake ambao tayari Rose alikuwa amewasaidia wakapiga kelele kwa nguvu, wakamkataza mwenyekiti asimpige.
“Walimwambia kama atampiga Rose kwa ile sime, wao watakwenda nyumbani kwake kumlaani, wakasema naye ni binadamu kama wengine na hakuna dhambi ambayo ameifanya na ana haki ya kwenda kijijini kwake kwa kuwa amezaliwa hapo, kwa hiyo zile kelele zilisaidia akaachiwa, lakini sisi kama ndugu tulikuwa tumeshakata tamaa kwamba wanamuua,” anasema Nayo.
Nayo anasema wakati mdogo wao anapambana kuvunja mila hizo kandamizi, hata wao walikuwa wanaishi kwa wasiwasi na kuitwa majina mabaya lakini kwa sasa baada ya mapinduzi, wote wanatamani wawe karibu nao na wanataka waunganishwe wawe karibu na Rose.
MWANAMKE KIONGOZI WA MILA
Kijoro Uyo ni miongoni mwa viongozi wa kimila wa kike waliochaguliwa mwaka huu, anasema licha ya Rose kupigwa vita, lakini ameonyesha ushujaa wa kupambana mpaka kuvunja ‘kigingi’ kilichowekwa enzi na enzi za mababu kwa jamii hiyo ya kimaasai na hata kufikia uamuzi wa kukubaliana naye kuingiza wanawake katika uongozi.
“Na mimi nilichaguliwa kuwa miongoni mwa viongozi hao sita wa kike ambao kwa sasa tunaingia kwenye vikao pamoja na viongozi wa kiume wa kimila na siyo kwamba tukiwa huko tunakaa kimya kama zamani, tunazungumza, wanatusikiliza na wanaamini hoja zetu nyingi tunazowaambia, kwangu mimi ni jambo kubwa sana,” anasema Kijoro.
“Tena Rose ametuhamasisha tunasimama kugombea kwenye siasa, tangu ametuelimisha tunasimama wengi wanawake kugombea, na sasa hivi nimesimama kugombea kwenye nafasi ya uongozi na nimechaguliwa kuwa mwenyekiti wa UWT kijiji cha Moroni Tarafa ya Loliondo, na sasa hivi ametupa mwongozo wa namna wa kuhamasishana kusimama kwenye uchaguzi wa serikali zaa mtaa, na wengi sana wanawake wameonyesha nia ya kugombea, kwa kweli bila yeye(Rose) tungekuwa bado tumelala,” anasema Kijoro.
Lengumo Parimilia, ni mmoja wa viongozi wa mila katika eneo hilo la Ngorongoro akitokea Kata ya Engarushorosamba, anasema wanamshukuru sana Rose kwa kusimama kwa nguvu kuwashawishi wakubali kuvunja mila waliyokuwa wanashikilia ya kutokuthamini na kumpatia nafasi mwanamke na kwamba tangu wakubaliane naye kuingiza wanawake katika jopo lao, wameanza kuona manufaa yake.
“Yaani muda mfupi tu baada ya kuwakubali wanawake kuingia kwenye uongozi tumeanza kuona manufaa yake, kwa miaka mingi sisi Malaigwanani wa eneo hili, hatukuwa na vitambulisho vya kututambulisha rasmi kwamba sisi ni viongozi, lakini sasa hivi Rose amepambana tumepewa na tumetambuliwa na serikali,” anasema Parimilia.
“Si hilo tu, lakini sasa hivi tumeanza kuona maendeleo kwenye wilaya yetu, sasa tunaitwa mara kwa mara wilayani kwenye vikao vya maendeleo wakati zamani wala hatukuwa tunakwenda, na kila tukienda kwenye vikao hivyo, wanawake tulionao kwenye uongozi ndio wanasimama kupeleka hoja na tunaona zinakubaliwa kirahisi sana na ni wepesi sana kuzungumza na ni wakweli mpaka tunaona kwamba tulikosea sana kuwazuia zamani.”
Parimilia anasema baada ya kuona matokeo mazuri na uwezo wa wanawake kwenye uongozi, sasa hivi wamewatangazia wananchi wote katika jamii yao kwamba hakuna kuwabagua tena wanawake katika jambo lolote na wametoa kibali rasmi kwa wanawake wote wanaotaka kugombea nafasi zozote za siasa wajitokeze na watachaguliwa kulingana na sera zao.
Anasema zamani wanawake walikuwa wakijaribu hata kusimama kuzungumza katika jambo lolote kwenye vikao au mikutano ya hadhara, wanatukanwa lakini kwa sasa wamepiga marufuku hilo na kwamba yeyote atakayesimama na kuwatukana watamchukulia hatua kali.
“Tumeona hakuna tena sababu ya kuwazuia maana uwezo wao tumeuona, wanafanya vizuri sana. Na kupitia uwezo wao ambao tumeona kwa muda mfupi, tukasema kumbe ndio maana sasa hivi Rais ni Mwanamke na anafanya vizuri, Spika wa Bunge naye ni Mwanamke na anafanya vizuri, na kuna mwanamke yuko hapa Ngorongoro anaongoza Jeshi la Polisi naye anafanya vizuri sana,
“Kwa hiyo tukasema mwanamke anayetaka uongozi kwenye vitongoji, udiwani au ubunge aende tu na hakuna wa kumtukana, atakayechaguliwa sawa na asiye chaguliwa sawa, washindane kwa uwezo wao,” anasema Parimilia.
OFISA MAENDELEO JAMII
Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ngorongoro, Daniel Bura, anasema kazi aliyofanya Rose na anayoendelea kufanya ni kubwa katika jamii na kwamba wao kama serikali wanaithamini kwa sababu inaisaidia serikali kuletea maendeleo wananchi wake.
“Kama mtu amepambana kuvunja mila ambayo ni kandamizi kwa watu wake na ambayo imewatesa miaka mingi, akatoa elimu ikaanza kubadilika licha ya kwamba ni aina ya jamii ambayo ina mifumo yake iliyoishikilia kwa nguvu, hilo ni jambo jema sana na tumeliona kwa Rose akifanikisha hilo.
“Pamoja na kwamba siyo rahisi kubadilika kwa haraka, lakini mpaka sasa amefanya kazi kubwa sana na inaonekana, kama ambavyo hakuna serikali inayopenda mwananchi wake ateseke, au aonewe, ametusaidia sana na tumeshirikiana naye sana katika kuhakikisha jamii ile inapata maendeleo na tunamtambua kwamba ni miongoni mwa watu wanaofanya vizuri sana kuleta maendeleo katika jamii yake,” anasema Bura.
TUZO ALIZOPATA
Rose anasema kupitia kazi ambazo amefanya amepata tuzo kadhaa ikiwamo kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, waandaaji wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Maendeleo ya Jamii mkoa wa Arusha pamoja na Ubalozi wa Ireland.
“Sijivunii kwa sababu bado naona kama sijafika, lakini mahali nilipo kwa sasa nimeona nimefika mbali, kwa sababu kwenye hii jamii wamefika mahali wakaamini uwezo wa mwanamke kwenye uongozi kama ilivyo kwa mwanamume, kwa hiyo sasa hivi mwanamke kusimama kugombea nafasi yoyote kwenye uongozi kwenye jamii ya kimasai na uongozi wa serikali siyo laana tena na hilo ndilo jambo nashukuru kila siku,” anasema Rose.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED