Kanisa Anglikana latoa tamko matumizi mabaya jina lake

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:52 AM Nov 06 2024
Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Mchungaji Canon Bethuel Mlula.
Picha:Mtandao
Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Mchungaji Canon Bethuel Mlula.

KANISA la Aglikana Tanzania limeomba serikali kupitia Msajili wa Jumuiya na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kuchukua hatua stahiki za kusitisha matumizi ya majina ya makanisa ambayo yanaiga yale yaliyokwishasajiliwa.

Ombi hilo linakuja huku kukidaiwa kuwa kumekuwapo na mpasuko mkubwa ndani ya kanisa hilo baada ya mchungaji mmoja kujiondoa na kuanzisha kanisa jipya ambalo limeondoka na makanisa saba ndani ya Dayosisi ya Mpwapwa.

Katibu Mkuu wa Kanisa hilo, Mchungaji Canon Bethuel Mlula, alitoa ombi hilo jana jijini hapa, wakati akisoma tamko kwa vyombo vya habari kuhusu kuanzishwa kwa kanisa jipya la Episcopal Anglican Province of Tanzania.

“Serikali kupitia Msajili wa Jumuiya na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, tunaomba kuchukua hatua stahiki za kusitisha matumizi ya majina ya makanisa ambayo yanaiga makanisa yaliyokwisha sajiliwa ikiwamo Kanisa la Free Anglican Church of Tanzania, Kanisa la Kiinjili la Aglikana na Episcopal Anglican Province of Tanzania,” alisema Canon Mlula.

Alisema serikali inapaswa kuzuia madhehebu ya dini matumizi ya majina yanayofanana jambo ambalo sio tu linaleta mkanganyiko, bali pia linafanywa kwa makusudi, ili kuwawezesha wale wanaoanzisha kujificha humo kupata waumini na kuwafanya mateka wa kiroho.

“Aidha, kutokana na uzoefu wa hivi karibuni wa baadhi ya makanisa yanayoanzishwa na wageni kutumia kudanganya Watanzania, tunaiomba Ofisi ya Msajili wa Jumuiya kufanya uhakiki wa kina madhehebu ya dini na wamiliki wake kabla ya kuamua kuyaruhusu kufanya huduma zake hapa nchini,” alisisitiza.

Aidha, alisema kwa kutambua haki ya kikatiba ya kila Mtanzania kuabudu pasipo kuvunja sheria wanaiomba serikali kulitazama kwa makini sana jambo hilo na kuchukua hatua stahili.

“Serikali ichukue hatua stahili za kuwakamata wamilikii wa Kanisa hili la Episcopal Anglican Church of Tanzania na makanisa mapya yenye kushabihiana na yale yaliyopo toka zamani kubadili mara moja majina yao pia kuzingatia sheria na taratibu za nchi katika kujiendesha,” alisema.

Kadhalika, alisema viongozi wa dini wanatoa rai kwa serikali kuweka mifumo madhubuti ya kuratibu haki za uanzishwaji wa jumuiya za kidini kwa nia njema ya kulinda amani, umoja na mshikamano wa Watanzania.

“Serikali itazame upya pia usajili wa makanisa ambayo yanashabihiana majina kwa kuwa baadhi ya viongozi wake wanatumia mbinu hiyo, ili kuwavuruga na kuwapotosha waumini na hatimaye kuwafanya watumwa wa imani,” alisema.

Vile vile, alisema kanisa linawajulisha waumini wote kubaki watulivu ndani ya kanisa lao wakati taratibu za ndani za kushughulikia suala hilo zinaendelea.

“Ijulikane pia kwamba kanisa la Episcopal Anglican Province of Tanzania kamwe si sehemu ya Kanisa Aglikana Tanzania wala Kanisa Aglikana Duniani,” alisema Canon Mulula.

Pia, alisema shutuma za masuala ya ushoga ambazo zinatolewa dhidi ya Kanisa Aglikana Tanzania na baadhi ya viongozi wanaoasi na kuanzisha makanisa mengine ni hoja ya kutaka kuichafua sifa ya kanisa.

“Kanisa Anglikana Tanzania halijawahi kuunga mkono masuala ya ushoga na hayo mambo ambayo yanaelezwa na baadhi ya wachungaji ambao wamekimbia na kuanzisha madhehebu yao ni hoja za kulichafua kanisa,” alisema Canon Mlula.