UTEKELEZAJI mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga umefikia asilimia 45.5 huku Watanzania 7,584 wakinufaika na fursa ya ajira.
Akizungumza jana jijini hapa wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma kuhusu utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati wa serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mratibu wa Mradi huo, Asiadi Mrutu, alisema kuwa hadi kufikia Septemba mwaka huu, Watanzania hao walinufaika na fursa hiyo ya ajira.
Alisema kwa kipindi hicho serikali imeingiza Sh. bilioni 10.69, ikiwa ni pango la ardhi ya mradi na kwa sasa maandalizi ya kulaza bomba ardhini yanaendelea.
"TPDC kwa kushirikiana na EACOP imetekeleza zoezi la uhamishaji makaburi kwenye eneo la Mkuza ambapo hadi sasa makaburi 1,146 yamehamishwa na huu uhamishaji makaburi umekuwa shirikishi na unaozingatia taratibu za nchi na za kimataifa," alisema.
Alisema kwa kila kaburi, kiasi cha Sh. 300,000 kililipwa kama rambirambi ili kuhamishwa.
“Zoezi la kuhamisha makaburi lilikuwa shirikishi na kushirikiana na familia na mradi uliheshimu sana hizo taratibu kwenye eneo la Igunga tulishindwa kuhamisha matatu na kusababisha njia ya bomba kuhamishwa.
"Tulikaa na jamii wakasema wanayatumia yale makaburi kufanya mila, wale walikuwa viongozi wao, Hanang' pia tumeacha kaburi moja kutokana na masuala ya kiutamaduni," alisema.
Aliongeza kuwa serikali inaendelea kushirikiana na mradi kuhakikisha makaburi mapya yanayobainika kwenye maeneo ya mradi yanahamishwa kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu fidia, mratibu huyo alisema kuwa hadi Septemba 30 mwaka huu, wananchi 9,858 kati ya 9,927 wametia saini mikataba ya fidia na Sh. bilioni 35.1 sawa na asilimia 99.3 zimelipwa.
"TPDC kwa kushirikiana na EACOP na serikali za mitaa inaendelea kufuatilia wananchi 69 waliobaki ili kukamilisha taratibu za kutia saini mikataba yao ya fidia na hatimaye kulipwa stahiki zao," alisema.
Akizungumzia kuhusu mapato, mratibu huyo alisema serikali inakadiria kupata mapato ya zaidi ya Sh. trilioni mbili kupitia mradi huo.
Alisema mradi huo utapita katika mikoa minane na vijiji 225 na kwa upande wa Tanzania, bomba litakuwa na urefu wa kilomita 1,147, mradi ukitarajiwa kukamilika Julai 2026.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TPDC, Marie Msellemu, alisema mafunzo ya utekelezaji mradi huo ni muhimu kwa waandishi wa habari ili kurahisisha kufikisha elimu kwa umma kutambua fursa zinazoambatana na mradi.
"Katika ushirikishwaji wazawa kwenye mradi, wamechangamkia mradi na wamekuwa wakishiriki kwenye fursa za mradi ili kujikwamua kiuchumi na kuongeza ukuaji uchumi wa taifa. Wanawake wamejitokeza kwa kiasi kikubwa kuchangamkia fursa," alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED