Je, wajua athari za kusafisha pasi yako kwa dawa Paracetamol?

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 06:42 PM Nov 05 2024
Pasi.
Picha:Mtandao
Pasi.

UPO utamaduni uliojengeka kwa baadhi ya watu kutumia kidonge cha ‘paracetamol’, ili kuondoa uchafu ulioganda kwenye pasi zao.

Utaratibu huo unatajwa kuwa una athari hasi kiafya, kutokana na moshi unaotoka kwenye pasi wakati wa mchakato wa usafishaji.

Mfamasia Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya, Msafiri Kiwanga, amesema hayo wakati akizungumza na redio Clouds, leo.

“Unapopiga pasi ukaunguza nguo yako inatengeneza kama ‘oil’ ambayo imegandia katika pasi yako maana yake unatakiwa kuisafisha pasi yako.

“Unahitajika kutumia bidhaa ambazoi zimeidhinishwa rasmi, kutumia paracetamol kusafisha pasi, kwanza ni hatari kwa afya yako unaweza kuapata madhara kutokana na moshi unaotoka wakati unasafisha na dawa hiyo.

Wakati kile kidonge kinayeyuka kinasababisha harufu fukani ambayo sio nzuri kiafya na kukusababishia kama kikohozi na ukashindwa kupumua vizuri. Kama utakuwa unaji-expose kwenye huo moshi kwa muda mrefu, maana yake utakuwa chronic,” amesema mfamasia huyo.

Alisema badala yake, wito kwa jamii kutumia njia tofauti, ili kuweka pasi zao safi kwa kutumia hatua ambazo zimeruhusiwa kitaalamu akitaja ipo njia ya kusugua pasi kwa kutumia ‘steel wire’.

“Unaweza kusugua kwa kutumia ‘baking powder’ amabyo imechanganywa pembeni kwanza na maji. Alafu ukaja kuigandisha kwenye pasi yako, baadae ukija kusugua uchafu utatoka.

“Pia unaweza kutumia ‘vinegar’ ambayo kemikali ya zenye acid, pia bidhaa ya kuondolea rangi kwenye kucha ‘remover’ inaweza kukusaidia. Hata dawa ya meno inasaidia, ikishaganda baadae unasafisha pasi,” anasema.