WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Ubunifu wa Afrika Kusini, Dk Bonginkosi Nzimande amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa teknolojia ya anga kati ya Tanzania na Afrika Kusini.
Dk Mzimande aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ziara yenye lengo la kukuza ushirikiano wa elimu kati ya mataifa hayo mawili.
"Tuna hamu ya kushirikiana katika maeneo mengi, hususan katika sayansi ya anga na teknolojia, ambayo inaendana na mwelekeo wa Taasisi ya (DIT)," alisema Dk Mzimande.
Alisisitiza kuwa tayari makubaliano yameanzishwa kati yake na Waziri mwenzake wa Tanzania Prof Adolph Mkenda ili kuchunguza zaidi maeneo ya ushirikiano.
"Tunataka kufanya kazi pamoja katika mipango, hasa katika teknolojia ya satelaiti, kwa matumaini kwamba hii itatufungulia njia ya kurusha satelaiti kwa pamoja," aliongeza.
Alihusisha nafasi hiyo na uwezo wa hali ya juu wa Afrika Kusini katika nyanja hiyo na akaonyesha shauku ya kutoa msaada kwa Tanzania.
"Tuna furaha zaidi kufanya kazi na Tanzania kwa sababu Afrika Kusini inataka kuona nchi nyingi za Afrika zikijihusisha na sayansi na teknolojia ya anga," alisema.
Waziri huyo alisisitiza umuhimu wa kuelimisha jamii za Afrika kuhusu jukumu la sayansi katika maisha ya kila siku ili kupata uungwaji mkono wa umma kwa mipango ya kisayansi.
"Tunahitaji kuhakikisha kuwa jamii inaelewa umuhimu wa sayansi kwasababu bila uelewa huo, hatuwezi kutarajia uungwaji mkono wao,” alisema.
Dk Mzimande aliahidi kuwa Afrika Kusini itaiunga mkono Tanzania, hasa katika kujenga uwezo kupitia kubadilishana wafanyakazi na wanafunzi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Dk Richard Masika alisifu ziara hiyo kama hatua muhimu kuelekea mipango kabambe ya Tanzania ya kurusha satelaiti tatu ndani ya miaka michache ijayo.
"Kwa msaada wa serikali, DIT tayari imeanzisha hatua za kurusha satelaiti yake ya kwanza mwaka 2026, ikifuatiwa na nyingine mbili mwaka 2027 na 2028," alisema, akibainisha kuwa ziara hiyo ilitoa fursa ya kipekee kwa DIT kuongeza utaalamu wa hali ya juu wa Afrika Kusini katika teknolojia ya anga.
Dk Masika alisisitiza kwamba DIT imejitolea kuoanisha mafunzo ya wanafunzi na mahitaji ya sekta.
"DIT inaunga mkono malengo ya kitaifa kwa kuendeleza wahandisi wenye uwezo kupitia mbinu inayozingatia uwezo badala ya nadharia pekee," alisema.
Alifafanua zaidi kuwa mbinu ya kiwanda cha kufundishia ya DIT inawapa wanafunzi ujuzi wa vitendo, na kuwafanya kuwa tayari soko baada ya kuhitimu.
Mkurugenzi wa Taaluma wa DIT, Dk Petro Pesha alisema DIT imekuwa na maono ya kusaidia mipango ya serikali kuhusu teknoojia ya anga.
Alisema moja ya jitihada walizofanya ni kufanikiwa kuanzisha idara ya anga mwaka 2023, na kuanzisha kituo cha teknolojia ya anga mwaka 2024, na kujiandaa kwa kurusha satelaiti yake ya kwanza chini ya mpango wa KiboCube mnamo Agosti 1, 2026.
Alifichua kuwa DIT imetembelea Urusi na Uchina ili kukusanya maarifa na kujenga uwezo wa ndani kwa ajili ya uzinduzi huo.
Dk Pesha pia alijadili faida pana za teknolojia ya anga, kutokana na mafanikio ya kiuchumi na uboreshaji wa ufuatiliaji wa kilimo ili kuimarisha usalama wa mpaka.
Dk Pesha alisisitiza kwamba teknolojia ya anga inachangia kulinda mipaka na wanyamapori, kupunguza gharama zinazohusiana na usalama wa taifa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED