WIZARA ya Afya imetaja sababu nne zinazochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la wagonjwa wa figo nchini kuwa ni pamoja na matumizi holela ya dawa za maumivu.
Naibu Waziri, Dk. Godwin Mollel aliyasema hayo jana bungeni alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Sylvia Sigula ambaye alitaka kujua chanzo cha ongezeko la wagonjwa wa figo nchini.
Dk. Mollel alisema ongezeko hilo pia linachangiwa zaidi na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, hususani shinikizo la damu na kisukari.
Alitaja sababu nyingine ni matumizi holela ya dawa, hasa za maumivu, watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU) wasiokuwa na ufuasi mzuri wa dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo na kutozingatia mtindo wa maisha unaofaa hususani matumizi makubwa ya chumvi, tabia bwete na matumizi ya vilevi, hasa pombe na bidhaa za tumbaku.
Naibu Waziri Mollel alisema serikali inaendelea kutoa elimu na kuasa jamii kuhusu kujikinga kwa kubadili mtindo wa maisha, ambao unajumuisha ulaji usiofaa hususani matumizi makubwa ya chumvi, vyakula vyenye sukari nyingi au nafaka zilizokobolewa.
Alisema serikali imeimarisha huduma za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza pamoja na matibabu ya VVU/Ukimwi ili kuzuia madhara ya magonjwa hayo.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Jacquline Kainja, alihoji mpango wa serikali kudhibiti matumizi holela ya dawa za binadamu ambazo zimeonekana kuwa moja ya sababu zinazochangia maradhi ya figo.
"Nini mpango wa serikali kuwezesha hospitali zake kutoa huduma ya kusafisha figo na kuwaondolea adha wagonjwa kwenye upatikanaji huduma na gharama za matibabu?”mbunge huyo alihoji.
Naibu Waziri Mollel, akijibu maswali hayo, alisema serikali inaendelea kuelimisha jamii kuhakikisha matumizi ya dawa yanazingatia maelezo ya daktari na mtu anapokwenda kununua dawa kwenye duka la dawa, awe ameandikiwa na daktari.
Hata hivyo, alisema katika kuwapunguzia wananchi mzigo wa matibabu ni suala la bima ya afya kwa wote na serikali inaimarisha upatikanaji vifaa tiba na dawa kwa kununua moja kwa moja viwandani badala ya kununua kwa watu wa kawaida.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Cecilia Pareso alisema gharama za kusafisha figo katika hospitali binafsi na za serikali zina utofauti wa bei.
"Ukienda kusafisha figo hospitali za binafsi ni nafuu kushinda hospitali za serikali, ni ghali! Nini mkakati wa serikali kupunguza gharama hizi ili wagonjwa wapate unafuu na matibabu?" alihoji.
Dk. Mollel, akijibu swali hilo, alisema hospitali za serikali zinatakiwa kuwa na gharama nafuu na kuahidi kulifuatilia suala hilo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Kunti Majala alihoji kama serikali iko tayari kupunguza gharama za usafishaji figo kutoka Sh. 300,000 hadi Sh. 50,000 kutokana na mchakato wa bima ya afya kwa wote kusuasua.
Naibu Waziri Mollel, akijibu swali hilo, alisema kuna uzinduzi mkubwa wa mpango huo wa bima ya afya kwa wote umefanyika jijini Arusha hivi karibuni na ni kiashiria cha kuanza kutekelezwa kwa suala hilo ili watanzania wawe na uhakika wa matibabu.
Alisema kuna timu inafanya kazi kuhakikisha gharama hizo zinapungua.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED