CHADEMA: Hata tukibaki na mgombea mmoja, hatujitoi Uchaguzi wa S/Mitaa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:20 AM Nov 06 2024
Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila.
Picha:Mtandao
Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila.

UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umesema utashiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hata kama kitabakiwa na mtaa mmoja baada ya orodha ya wagombea kuwekwa hadharani.

Umesema hata kama kukitokea changamoto kubwa kiasi gani katika hatua zilizobaki, hakitakuwa tayari kujitoa katika uchaguzi huo.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Arusha na viongozi wa chama hicho, wakiwamo Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.

Kigaila alisema kuwa tangu kufunguliwa mlango wa kuchukua na kurejesha fomu, kumekuwa na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo, wanaendelea kuzifanyia tathmini na watatoa taarifa ya jumla na hatua za kuchukua. 

"Lakini ninaomba niwaambie wanachama wetu kwamba pamoja na chagamoto zilizojitokeza, hatutarudi nyuma kama tulivyofanya mwaka 2019. Niwasihi endeleeni kujiandaa, hatutajitoa. 

"Tunaendelea kufanya tathmini katika kanda zote nane, tutatoa taarifa kamili kuhusu changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye kazi hii ya kuchukua na kurejesha fomu, lakini hata iweje uchaguzi ni lazima tushiriki," alisisitiza Kigaila.

Kwa upande wake Lema alisema sekretarieti ya chama hicho hivi sasa inakusanya taarifa nchi nzima juu ya mwenendo wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa wagombea wake kwa ajili ya kukabidhi kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe.

"Baada ya kumaliza kukusanya, tutakabidhi kwa mwenyekiti wetu taifa halafu yeye ndiye atatoa taarifa kamili kwa umma.

"Lakini hata hivyo, kwa wanachama wetu na viongozi wetu kila mahali, wasikate tamaa kuendelea kupigania dhamira yetu. Hata kama tutabaki na wenyeviti watano, na wengine wote kuenguliwa, tutafanya kampeni kama vile tumebaki nao asilimia 90 kama ambavyo tulikuwa tumepanga.

"Chama chetu kabla ya kuanza kuchukua na kurejesha fomu, tulikuwa na wagombea kwa asilimia 87 hadi 92 nchi nzima, wito wangu kwa viongozi wote wa kanda wa chama chetu ni kwamba, hata kama tukibaki na mgombea kwenye mtaa mmoja, twende naye tukafanye kampeni.

"Hatuendi tu kufanya kampeni kwa sababu tunataka kushinda, tunataka kikombe cha dhambi kijae. Na mimi nimefunga na kuomba kwa ajili ya suala hili," Lema alidai.

Kauli hiyo ya CHADEMA imekuja siku moja baada ya Chama cha ACT Wazalendo kusema kinajiandaa kuandika barua kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutaka kurejeshwa katika mchakato wa uchaguzi huo, wagombea wa chama hicho waliokumbana na changamoto wakati wa kuchukua na kurejesha fomu, ikiwamo ofisi husika kunakorejeshwa fomu hizo kutofunguliwa makusudi ili kuwanyima haki yao ya kikatiba.