BAADHI ya kampuni za wazawa zinazotoa huduma kwa Kampuni ya Shanta Mining, zimeilalamikia kwa kusitisha mikataba nao pasi na kuwapa taarifa.
Kampuni hizo zimedai kuwa zimekuwa zinatoa huduma na vifaa kwa kampuni hiyo ya madini kwa muda mrefu, lakini huu ni mwezi wa tatu hazijapewa kazi (zabuni).
Kutokana na madai hayo, Waziri wa Madini, Antony Mavunde ametuma timu ya watalaamu wa wizara kuchunguza undani wa suala hilo.
Mmoja wa wamiliki wa kampuni hizo (jina tunalihifadhi) aliiambia Nipashe juzi kuwa wamepata taarifa zisizo rasmi kwamba kampuni zao zimewekwa katika orodha ya kutopewa kazi (blacklist) na Kampuni ya Shanta Mining, pasi na kuambiwa kilicho nyuma ya uamuzi huo.
"Sisi tunatambuliwa hadi kwenye Tume ya Madini kwamba tunaipa huduma kampuni hiyo, maana sheria za nchi zinaelekeza kampuni za madini zinapokuwa zinahitaji vifaa au huduma inayozidi Dola 100,000, lazima makubaliano hayo yapitie kwenye Tume ya Madini.
"Tunashangaa kampuni zetu zimeondolewa kwenye orodha ya kupewa kazi za Shanta. Sasa kazi zote anapewa ... (akataja jina la kampuni). Tunajua kampuni hii imesajiliwa Tanzania, lakini wamiliki wake wana asili ya India," alidai.
Aliendelea kudai kuwa hatua iliyochukuliwa ya kuwanyima kazi wazawa, wanahisi italeta madhara si tu kwa kampuni zao, bali hata katika mapato ya madini kutokana na ukiukwaji utaratibu wa 'local content'.
Waziri wa Madini, Mavunde, alipotafutwa na Nipashe jana asubuhi kuzungumzia suala hilo, alisema hakuwa na taarifa za kinachojiri katika Kampuni ya Shanta, hivyo akaomba apewe muda afuatilie.
Baada ya saa moja, Waziri Mavunde alitoa mrejesho kwa mwandishi, akisema "nimeelekeza timu yangu kujiridhisha juu ya usahihi wa taarifa hizo".
Honest Mrema, Mkuu wa Operesheni wa Shanta Mining, alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia suala hilo, alikiri kampuni yao kusitisha kutoa kazi (zabuni) kwa baadhi ya kampuni za wazawa.
Alisema uamuzi huo imechukuliwa na uongozi wa kampuni ili kupisha uchunguzi wa kihasibu unaoendelea dhidi ya baadhi ya kampuni ambazo wamezihisi kufanya udanganyifu wa kifedha.
Mrema alifafanua: "Hivi karibuni, Shanta imekuwa inaendelea na ukaguzi wa ununuzi na baadhi ya masuala kuhusu ubora, bei na udanganyifu wa kifedha umegundulika.
"Kazi hii bado inaendelea na ripoti kamili itakapotolewa, itawasilishwa pia kwa Tume ya Madini. Kwa sasa, baadhi ya malipo yamezuiwa hadi matokeo ya uchunguzi yatakapojulikana.
"Baadhi ya wauzaji kama vile ... na ... (alitaja majina ya kampuni mbili) wameathirika, na majadiliano yanaendelea kutafuta suluhisho.
"Shanta imejizatiti kutumia wauzaji wa ndani kwani ni faida kubwa, na inahakikisha inazingatia kikamilifu kanuni za 'local content' (kutumia wazawa au kampuni za wazawa katika kupata huduma au vifaa)."
Alipoulizwa na Nipashe kuhusu kampuni inayolalamikiwa kwamba hivi sasa wanaendelea kuipa kazi/ zabuni ilhali wazawa wengine wananyimwa, Mrema alisema "si kampuni zote zinatiliwa shaka. Zipo nyingine zaidi zinaendelea na kazi".
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED