TANROADS yatoa ufafanuzi bil. 18/- za matengenezo miundombinu BRT

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:26 AM Nov 06 2024
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo.
Picha: Mtandao
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo.

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam unatekeleza mradi wa matengenezo ya miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) awamu ya kwanza chini ya mradi wa OPBRC uliotiwa saini rasmi tarehe 7 Septemba 2018.

Mradi huu ni wa muda mrefu; ulianza rasmi tarehe Mosi Aprili 2019 ukitekelezwa na mkandarasi M/s Bharya Engineering & Contracting Co. Ltd (BECCO) kwa muda wa miezi 60, yaani miaka mitano.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo, alitoa ufafanuzi huo jana na kueleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Sh. bilioni 18.509 ambazo zinajumuisha makundi matatu ya kazi na si mradi wa Jangwani pekee.

Aliyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na mradi wa matengenezo ya miundombinu ya mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 21.4 ukihusisha barabara ya Morogoro kuanzia Ferry mpaka Kimara Mwisho, barabara ya Kawawa (Magomeni Mapipa – Morocco) na barabara ya Msimbazi (Fire – Msimbazi BRT Station). 

Mkumbo alisema kuwa TANROADS pia inatekeleza kazi za maboresho ya sehemu zilizoharibika, ikihusisha matengenezo makubwa ya tabaka la lami katika sehemu zilizokuwa zimeharibika. 

Maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni Ubungo Maji, Kibo, Corner, Baruti, Bucha, Korogwe na Kimara Mwisho. Tabaka la lami katika maeneo haya liliondolewa (milling) pamoja na kuwekwa lami mpya kwa kutumia teknolojia ya Superpave (SP 12.5), kuweka nguzo za zege (precast concrete poles C20/guard posts), ujenzi wa sehemu za watembea kwa miguu (paving blocks), ujenzi wa kingo za barabara (kerbstones) na matengenezo kwenye njia za waendesha baiskeli. 

Alisema TANROADS Dar es Salaam pia imefanya kazi za dharura. Kazi hizi zinahusisha matengenezo ya uharibifu ambao haukutarajiwa. Kazi hizi ni pamoja na kuondoa tope, mchanga na takataka kwenye daraja na eneo la barabara wakati wa mafuriko na mvua kubwa na matengenezo ya miundombinu yatokanayo na ajali za barabarani kwenye miundombinu ya BRT awamu ya kwanza. 

Mkumbo alieleza kuwa kazi za matengenezo zimefanyika wakati wote. Kazi hizo zinahusisha; urudishiaji wa michoro ya barabara (road marking), uwekaji wa alama za barabarani, matengenezo/uzibuaji mitaro ya maji ya mvua ndani ya uwanda wa Km 21.4 za mradi, kuweka mifuniko ya zege kwenye mifumo ya maji, kuondoa mchanga kwa kufagia barabara ndani ya Km 21.4 kila siku. 

Kazi zingine, meneja huyo alisema ni pamoja na kufyeka majani na kutunza maeneo yenye bustani ndani ya eneo la mradi, kuondoa vichaka na kupunguza miti iliyo pembezoni mwa barabara, kuziba viraka/mashimo, matengenezo madogo ya madaraja yaliyomo ndani ya mradi, marekebisho ya njia za waenda kwa miguu/baiskeli, matengenezo ya nguzo za zege zinazoharibika, matengenezo ya maungio ya zege, marekebisho ya mifuniko na kuzibua mifereji yote iliyo katika eneo la mradi.