Mwembe Makumbi City yatakata Ligi Kuu Z'bar

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 08:22 AM Nov 06 2024
Mwembe Makumbi City.
Picha: Mtandao
Mwembe Makumbi City.

PAMOJA na ugeni wao kwenye Ligi Kuu Zanzibar timu ya Mwembe Makumbi City, imerejea katika kasi yake ya ushindi baada ya juzi kuibuka na ushindi.

Mwembe Makumbi City, ambayo huu ni msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Zanzibar, juzi Jumatatu ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Chipukizi FC, mchezo huo ukichezwa katika Dimba la Mau ze Dong majira ya saa kumi alasiri na kujaza mashabiki wao wengi waliombatana na kikundi kilichokuwa kikitoa burudani ya ngoma.

Kwa ushindi huo sasa Mwembe  Makumbi City wamerejea katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu baada ya kufikisha pointi 19.

Nafasi ya tatu inashikiliwa na Mlandege FC yenye pointi 17 huku kinara wa ligi hiyo Mafunzo FC ikiwa na alama 20.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mchezo huo, Kocha wa Mwembe Makumbi City, Rajab Mrisho Rajab, alisema kufanya vizuri kwa timu hiyo kunatokana na hamasa kubwa waliyonayo wachezaji wake.

Alisema licha ya kupoteza mchezo wao uliopita, lakini wachezaji walicheza kwa ari na hamasa kubwa ya kupata matokeo.

Rajab alisema katika mchezo wa juzi dhidi ya Chipukizi FC, ulikuwa mgumu licha ya kufanikiwa kukata kiu yao kwa kupata pointi hizo tatu.

Alisema wapinzani wao walikuja na mpango wao wa kupata matokeo chanya baada ya kupoteza mchezo wao wa nane, lakini pia na wao walikuwa na malengo kama yao kutokana na kudondosha pointi zote tatu mechi iliyopita.

“Tumefanikiwa kupata pointi tatu katika mchezo huu mgumu, wachezaji walipambana kuona tunafanikiwa lengo letu, lakini haikuwa kazi rahisi,” alisema.

Alisema kikosi chake kinaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo wao wa 10 ambao watashuka uwanjani kesho kuvaana na Junguni FC.