DIT inapobeba dhamana kuacha mkaa ikishikwa mkono na serikali, UNDP

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:42 AM Mar 28 2024
Wafanyabiashara wa mkaa, Mbande, Dar es Salaam wakisubiri wateja.
Picha: Maktaba
Wafanyabiashara wa mkaa, Mbande, Dar es Salaam wakisubiri wateja.

WATANZANIA takribani 33,000 mijini na vijijini, wanaelezwa kuwa wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati chafu inayohusisha kuni, mkaa na vinyesi vya wanyama kama ng’ombe kupikia.

Idadi hiyo inayopotea ni kutokana na kuumwa maradhi yanayoshambulia mfumo wa hewa unaohusisha koo, mapafu, pia na midomo wakati mwingine wakiumwa saratani na kichomi. 

Vifo na athari hizo ni matokeo ya kutumia nishati chafu kwa miaka mingi, vinaelezwa na mtaalamu wa matumizi bora ya nishati kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Sayuni Mbwilo, katika mazungumzo na Nipashe.

Anasema, chanzo cha magonjwa na vifo ni vumbo na moshi unaotokana na kutumia kuni, mkaa, mabaki ya mimea, vinyesi vya ng’ombe na mbuzi.

Aidha, kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, takriban asilimia 85 ya Watanzania wanatumia nishati ya kuni, mkaa, mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama, huku asilimia 72 ya nishati yote iliyoko nchini ikitumika majumbani na si viwandani au kwenye usafirishaji.

Katika kutekeleza mradi wa kubadilisha matumizi ya nishati duni, serikali na wadau wanamlenga zaidi ‘mama’ .

Wizara ya Nishati, UNDP, Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) wamechukua hatua za kimkakati kutafiti na kutoa suluhisho la kuepukana na nishati chafu jikoni.

Hapo ni kuhamasisha jamii hasa wanawake kuachana na kutumia kuni na mkaa jikoni na kuhamia kwenye gesi, umeme na mkaa mbadala ni moja ya mikakati hiyo, ambayo itafanikisha kutunza mazingira na kulinda afya za wananchi.

Sayuni anafafanua kuwa, Watanzania hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi, kama gesi, umeme, sola, mkaa mbadala na au vimiminika kama ‘etheno’.

Anasisitiza elimu hiyo ni muhimu kwenye nishati, kwakuwa ikikosekana watu hawataelewa jinsi jiko sanifu linavyosaidia kuepuka matumizi ya kuni, mkaa au mabaki ya mimea kupikia ambayo pamoja na kudhuru mapafu na koo, pia huchangia uharibifu wa mazingira na tatizo la mabadiliko ya tabianchi.

Anazungumzia hatua zinazochukuliwa na UNDP akitaja kugharamia masomo ya wanafunzi wa kike 10 kujifunza mafunzo ya nishati safi kwa ngazi ya shahada katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na kwamba, baada ya kuhitimu watatumika kukuielimisha jamii umuhimu wa nishati salama.

Pamoja na mafunzo, DIT imepokea vifaa vya kisasa vya kufundishia pamoja na kupima ufanisi, viwango na matumizi sahihi ya majiko hayo.

“Wanawake 10 watakwenda kuvitumia vifaa hivi kujua namna gani wanamsaidia Mtanzania, hasa mama ile nishati yake safi ya kupikia isipotee bali itumike kwa ufanisi, umakini na ubora,” anasema Sayuni na kuongeza Ubalozi wa Ireland, umeongeza msaada wa uhisani wa masomo kwa wanafunzi wengine 10 wanawake 

Mmoja wa wanafunzi wanufaika wa ufadhili huo, Sherida Magomere, anasema ujuzi watakaopata utawaelimisha Watanzania umuhimu wa nishati salama ya kutumia katika shughuli za kila siku na hasara za nishati chafu ili waepuke madhara.

Mkufunzi Mwelekezi kutoka DIT, Mawazo John, anasema, kuanza kwa mradi huo kumeleta mwamko kwa wanafunzi wa kike kujiongezea uelewa katika eneo la nishati safi, akibainisha awali katika darasa nzima wanawake walikuwa wanne pekee, lakini mwaka huu wako zaidi ya 40 wakiwemo wanaogharamiwa na UNDP.

Augustino Masse, mtaalamu wa teknolojia za nishati kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), anasema jamii inahitaji elimu ya kutambua inaathirika vipi na nishati isiyo safi.

Hapo anatoa mfano wa afya kwamba, inachukua miaka mingi kupata athari za moshi na vumbi jembamba analivuta mtu kutoka kwenye kuni, mkaa na mabaki ya mimea, kwenye shughuli zake.

“Leo anaweza asione kwamba nishati safi ni kitu muhimu, lakini tukielimisha jamii ipasavyo, unaposema nishati safi unamaanisha nini tutafikia lengo.

“Cha kwanza ni mtu aelewe na aone maana ya kuhusika kwasababu hili ni jambo linalohusisha kila mmoja wetu na pia maisha yetu,” anaeleza Masse.

“Mimi ni mtaalamu lakini kama mwananchi haelewi umuhimu wa hili utaalamu wangu utakuwa haujafanya chochote, ndio maana nasisitiza cha kwanza ni elimu na uelewa kwa jamii. 

‘Chini ya mradi huu kuna kipengele kimewekwa mahususi kwamba watu waelimishwe, kwenye viwanda, nyumbani na kote ambako nishati inatumika,” anaongeza.

Anasema pamoja na kuhimiza kuacha kuni na mkaa, TIRDO imefanya tafiti na kubaini namna bora ya kutengeneza mkaa mbadala, utaalamu wanaoendelea kuupelekea kwa Watanzania wengine maeneo mbalimbali.

UHAKIKI MAJIKO

Mtaalamu huyo wa teknolojia kutoka TIRDO, anasema nishati safi, inaanzia kwenye jiko, akibainisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS), majiko yanatakiwa kuwa katika daraja la kwanza yakiwa na ufanisi wa asilimia 50, la pili zaidi ya asilimia 40 na tatu zaidi ya asilimia 30, nne kuanzia asilimia 20 hadi 29. 

Anasema, kutokana na viwango hivyo wanaendesha zoezi la uhakiki ubora na kuwasaidia na kuwashauri namna ya kuboresha majiko yao.

Winifrida Robert ni Mhandisi wa Nishati kutoka TIRDO, anayesema wanawake wengi wanapata madhara ya kiafya na kuingia gharama kubwa za matibabu, kwa kutokujua ufanisi wa jiko analolitumia na kusisitiza uelewa wa suala hilo kuwa ni muhimu kusaidia kutumia nishati kwa kiwango.

 “TIRDO kwa kushirikiana na UNDP imetengeneza maabara yenye vifaa vya kisasa vinavyotumika kupima ufanisi na hewa ukaa ambayo inatoka kwenye jiko, wazalishaji wengi hawajui maana ya kupima ufanisi wa jiko, pia wanunuzi hawaelewi kuna faida unayoipata kwa kununua jiko lenye ufanisi.

“Chini ya mradi tumewafikia baadhi ya wajasiriamali na wameleta majiko yao kupimwa, hivyo nitoe wito kwa wazalishaiji wengine kufika TIRDO kupima ufanisi na tutawapa ushauri kuongeza thamani ya bidhaa zao. Pia watu kabla ya kununua wajiridhishe kuhusu ubora,”anashauri Winifrida.