WIZARA ya Fedha,imesema kuwa kuna changamoto kubwa ya wastaafu kutapeliwa mtaani,huku wakiitaka jamii kuchukua tahadhari na kufuata njia sahihi katika kupata huduma.
Akizungumza Novemba 7,2024, wakati wa kongamano kati ya Wizara ya Fedha na Wahariri wa vyombo vya habari, Ofisa Mwandamizi Kitengo cha Pensheni Wizara ya Fedha,Ushindi Kalinga, amesema wanapokea malalamiko mengi ya wastaafu kutapeliwa na watu wanaojitambulisha wametoka wizarani.
"Ili kukabiliana na utapeli wanamtumia ujumbe mfupi mstaafu kwamba amelipwa kiasi fulani na kama ana changomoto yoyote awasiliane na wizara kwa namba iliyowekwa wazi,"amesema.
"Huduma zinazoyolewa na serikali ni bure,ishara kwamba ni utapeli ni pale unapotakiwa kutoa fedha ili uhudumiwe sijui Stemp Duty, hiyo ni alama ya utapeli na sio serikali,"amesema.
Kalinga, amesema wanashirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Jeshi la Polisi Tanzania, Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI) ili kuwatambua na kuchukua hatua kwa wanaowatapeli wastaafu.
"Wazee wetu wengi wanatapeliwa,wengi wameumizwa huko mtaani.Pamoja na polisi kufanyakazi lakini ni wajibu wa kila mmoja kujilinda kwa kutokubali kutotoa taarifa zake wala kutoa ushirikiano kwa watu wanaotaka kulipwa ndio wapate huduma," amesema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED