WATU wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa mashtaka ya kumuua kwa kukusudia mtoto Greyson Kanyenye (6) katika mtaa wa Ilazo, jijini Dodoma Desemba 25 mwaka huu.
Hao ni Kelvin Joshua (27) na Tumaini Msangi (28) ambao wote walisomewa mashtaka yanayowakabili na Wakili Mwandamizi wa Serikali Patricia Mkina mbele ya Hakimu Mkazi Denis Mpelembwa.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Mkina alidai washtakiwa wote wawili walifanya kosa la mauaji ya Greyson Kanyenye, Desemba 25, mwaka huu kinyume cha vifungu namba 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mpelembwa alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mauaji, hivyo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani huko.
"Kosa la mauaji halina dhamana, hivyo mtarudi mahabusu hadi kesi yenu itakapotajwa tena Januari 13, 2025," alisema Hakimu Mpelembwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, akizungumzia tukio hilo Desemba 25 mwaka huu, alisema mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya nyumba ukiwa na majeraha shingoni.
Kamanda Katabazi alisema tukio hilo lilitokea saa moja asubuhi katika mtaa wa Bwawani, Ilazo Extension, jijini Dodoma, nyumbani kwa Ofisa Uvuvi wa Mtera, Hamis Mohamed.
Alisema kuwa siku hiyo, Hamis na mama wa mtoto Greyson walikuwa wametoka nyumbani kwa ajili ya matembezi, wakimwacha mtoto huyo chini ya usimamizi wa dereva bodaboda Kelvin.
Alidai kuwa bodaboda huyo alifahamika kwa familia ya mtoto huyo kupitia huduma ya usafiri anayotoa kwa familia yao.
"Bodaboda huyo aliachiwa mtoto ili amwangalie kipindi ambacho watakuwa kwenye matembezi, wawili hao wakati wa usiku waliporudi, mtoto hawakumwona hadi asubuhi majira ya saa moja walipomkuta katika chumba akiwa ameuawa, mwili ukiwa na alama za kupigwa na kitu kizito shingoni mwake," alisema.
Kamanda Katabazi alisema Jeshi la Polisi lilimshikilia bodaboda huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa tukio hilo la mauaji huku akitoa wito kwa wazazi kuacha tabia ya kukabidhi watoto wao kwa watu ambao hawawajui vizuri ili kuepusha matukio kama hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED