Watishia kushiriki uchaguzi kisa ukosefu wa umeme

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 07:09 AM Jun 20 2024
Sanduku la kupiga kura.
Picha: Mtandao
Sanduku la kupiga kura.

WANANCHI zaidi ya 1,300 kutoka vitongoji vya Nyamagana na Itulahumba wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe wamesema hawaoni sababu ya kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu, kutokana na vitongoji vyao kutokuwa na umeme.

Wakizungumza na Nipashe wananchi hao walisema licha ya uwepo wa mpango wa usambazaji wa umeme vijijini lakini katika kata yao bado vitongoji vyao havijafikiwa na umeme, licha ya vitongoji vya vijiji vingine jirani kufikiwa na huduma hiyo.

Walisema hawaoni umuhimu wa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu kwa sababu viongozi hawawapi ushirikiano.

Wananchi hao akiwemo, Alex Mhagama alisema hivi sasa watoto wao wanakosa masomo ya jioni kutokana na kukosekana kwa umeme.

“Kizazi cha sasa kinategemea sana elimu, kwa hiyo kama kiongozi anahitaji kuchaguliwa basi asimame na sisi kwa sababu tunahitaji umeme,” alisema Mhagama.

 Wema Mfilinge alisema kukosekana kwa umeme katika maeneo yao kunasababisha wakose huduma za msingi ikiwemo viwanda na kusababisha kutokukuwa kwa uchumi wao.

“Hata kwenye kusaga unga tunakwenda mashine za mbali sana. Wengine wana cherehani zinatumia umeme lakini wanashindwa kuzitumia kwa sababu hakuna umeme,” alisema Mfilinge.
 
 Diwani wa Kata ya Itulahumba, Thobias Mkane alisema ni kweli vitongoji hivyo havijafikiwa na mpango huo na kueleza kuwa jitihada zinaendelea ili kuhakikisha vinafikiwa na umeme.

“Mpaka sasa hivi kuna vitongoji havijafikiwa na umeme kabisa ni vitano lakini vingine vimefikiwa katika kata yangu, nina vitongoji 15, mpaka sasa hivi tumeshapeleka umeme kwenye vitongoji 11 kwa hiyo tumebakiza vitongoji hivi vinne ama vitano kwa ajili ya kuhakikisha tunamaliza,” alisema Mkane.

Naye Mratibu wa Miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) Wilaya ya Wanging'ombe, Justine Dickson alisema kwa awamu ya pili B vitongoji 75 ambavyo vimepitiwa na laini kubwa ya umeme vitafikiwa na huduma ya umeme jazilizi na kueleza kuwa mpango wa serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na umeme katika awamu ya pili C.