Wakili Nkuba ajinadi kurejesha heshima ya TLS

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 03:12 PM Jul 10 2024
WAKILI wa Kujitegemea Sweetbert Nkuba.
Picha:Mpigapicha Wetu
WAKILI wa Kujitegemea Sweetbert Nkuba.

WAKILI wa Kujitegemea Sweetbert Nkuba, amesema anahitaji kurejesha heshima ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), na kuwa nguvu moja kwa sababu kuna mambo mengi ambayo yanatishia na kuwagawa mawakili kutokana na shughuli wanazozifanya.

Aidha, amesema kuna baadhi ya wenye itikadi za vyama vyao wanataka kuihamisha TLS  kutoka kwenye uhalisia wake na kutaka kuifanya kuwa chama cha siasa jambo ambalo halikubaliki ni wakati wa familia hiyo kukaa pamoja.

Nkuba amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi kampeni zake na kutoa sababu kwanini achaguliwe kuwa rais TLS ili kurejesha heshima ya mawakili.

Amesema imefikia hatua wakili anayefanya shughuli za jinai wamekuwa maadui wakubwa na baadhi ya mawakili wengine, lakini pia kuna watu wenye itikadi za vyama vyao wanataka kukifanya chama hicho kuwa cha siasa.

"Kila mmoja anaitikadi yake chama chake na katika itikadi hizi mtu anaweza kubadilika muda wowote akatoka chama kimoja kwenda kingine sasa kama wanachama wa TLS tayari walikuwa na itikadi yako ya mwanzo je nao wahame tena kufata itikadi hiyo,"alihoji  

Wakili Nkuba amesema atakwenda kusimamia maslahi ya mawakili ili wakili aweze kulipa ada ni lazima kibali chake kifanye kazi anaposhindwa kulipia basi hapati maslahi tena.

"Nitakwenda kupambana na vishoka wote wanaobandika matangazo wakijiita mawakili hili hali sikweli na kufanya sifa ya mawakili kuwa mbaya,"amesema Wakili Nkuba

Amesema amelenga kusaidia vijana chipukizi ambao wamekuwa wakibaguliwa kwa kutopewa ushirikiano na mawakili wakongwe baada ya kuwa wameapishwa tayari kuwa mawakili,hivyo ataandaa ofisi itakayojumuisha mawakili wote.

Amesema TLS iliundwa kwa lengo la kuwaleta pamoja mawakili, kutetea na kusimamia haki zao bila kuangalia ukomavu au uchanga wa mtu yeyote.