Ustawi wa Jamii waanzisha mtaala mpya malezi, makuzi

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 07:10 PM Jul 09 2024
Ustawi wa Jamii waanzisha   mtaala mpya malezi, makuzi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Ustawi wa Jamii waanzisha mtaala mpya malezi, makuzi.

CHUO cha Ustawi wa Jamii kimetangaza kuanza udahili wa mtaala mpya wa malezi na makuzi ya awali ya mtoto ili kuleta tija katika jamii pamoja na kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto.

Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Benedict Nkwao, kwa niaba ya Mkuu wa Chuo, Dk. Joyce Nyoni, alitangaza hatua hiyo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 48 ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Alisema mtaala huo mpya mahususi unakwenda kusuka wakufunzi na wataalamu wa kwenda kufundisha walimu wa watoto, walezi wa watoto, ikiwamo kwenye vituo vya kulea watoto na vituo vya ‘daycare’ na makundi mengine yahusuyo watoto.

Nkwao alisema mtaala huo utatolewa kwa ngazi ya Cheti na Diploma katika Kampasi ya Kisangara Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Aidha, alifafanua kozi hiyo itakwenda kutoa suluhisho kusaidia kuwajenga kuhusu malezi ya watoto kwa kuwa jamii inakabiliwa na changamoto kubwa katika malezi hayo ikiwamo ukatili kwa watoto.

1

Mtaala huo utakwenda kuwaongoza katika ulinzi wa mtoto, kuwafundisha taratibu za kuwaongoza katika michezo ya watoto, saikolojia ya mtoto, sanaa na vingine vingi vinavyohusu makuzi ya mtoto kwa ujumla. 

Alifafanua tayari chuo kimeshaanza kudahili wanafunzi hivyo kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa hiyo, ili waweze kwenda kujiunga na kozi hiyo muhimu katika ustawi wa mtoto.

“Watanzania wanafunzi wenye uhitaji kutaka kujiunga kozi hii waje wajitokeze kwenye banda letu hapa hapa tunafanya usajili.”

Wakazi wa jijini Dar es Salaam waliyoongea na Nipashe walisema kuwa chuo hicho kimeona mbali kwa kuleta kozi hiyo mpya ambayo itakwenda kukomboa watoto shuleni na katika vituo vya watoto.

"Walezi watakuwa wamesukwa vya kutosha kuhusiana na malezi ya mtoto kwa ujumla," alisema Anna Rahael.

2