‘USAID mshirika muhimu Tanzania safari ya maendeleo kuelekea kipato cha kati’

By Mkurugenzi USAID Tanzania Craig Hart , Nipashe
Published at 01:25 PM Oct 30 2024
 Mkurugenzi Mkazi wa USAID nchini Tanzania, Craig Hart.
Picha: USAID Tanzania
Mkurugenzi Mkazi wa USAID nchini Tanzania, Craig Hart.

KWA zaidi ya miongo sita, Marekani, kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania, katika safari yake ya maendeleo kuelekea hadhi ya kipato cha kati na katika kuongeza wastani wa umri wa kuishi kwa miaka 16 katika miongo miwili iliyopita.

Marekani itaendelea kusaidia kudumisha mafanikio haya na mengine, pamoja na kuboresha afya na ustawi wa Tanzania.

Kama Mkurugenzi Mkazi wa USAID nchini Tanzania, najivunia kila siku kuona kazi za wafanyakazi wetu wote wakiwamo Wamarekani na Watanzania pamoja na washirika wanaotekeleza miradi yetu. 

Pia nafurahishwa na ushirikiano tuliojenga na sekta binafsi. Kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi na kuwawezesha wajasiriamali wa Kitanzania, ni muhimu katika kufikia maendeleo ya kiuchumi endelevu na jumuishi ambayo Watanzania wanastahili na kuyatarajia.

Mwaka uliopita pekee, USAID imetoa zaidi ya dola milioni 400 kama ruzuku ili kuimarisha biashara, kukuza ajira na kuchochea maendeleo nchini Tanzania. 

Nataka kusisitiza jambo hili fedha hizi ni ruzuku na sio mikopo; maana yake zimesaidia kuboresha afya, ustawi na kukuza fursa nchini Tanzania bila kuongeza mzigo wa deni la taifa kwa vizazi vijavyo.

Aidha, Shirika la Fedha za Maendeleo la Marekani (DFC) hivi karibuni lilitangaza mkopo wa moja kwa moja wa zaidi ya dola milioni 300 kwa Benki ya CRDB, ambao utawezesha zaidi ya biashara ndogo 4,500 kupata mikopo. 

Pamoja na uwezekano wa Tanzania kurejeshwa kwenye mpango wa ushirikiano kupitia Shirika la Changamoto ya Milenia la Marekani (MCC) na mipango mingine ya kiuchumi ya Marekani, mipango hii inaonyesha kujitolea kwa kina kwa Marekani katika kuwawezesha watu wa Tanzania na kuimarisha uchumi wa taifa.

Ushirikiano wa awali wa USAID umepata matokeo makubwa na sekta binafsi ya Tanzania, lakini ili kupata mafanikio makubwa zaidi hapana budi kusaidia biashara binafsi na wajasiriamali wa Kitanzania kuwa washirika katika maendeleo. 

Huu ndio ushirikiano utakaoleta matokeo ya kiuchumi ambayo kwa kiasi kikubwa yatazidi kile ambacho USAID na Marekani wanatoa kwa sasa kupitia ufadhili wa maendeleo. 

Tunajivunia kuona Prakseda Melkior, mkulima kutoka Morogoro, ambaye alitumia mafunzo aliopata kupitia USAID kukuza biashara yake, kupanua shamba lake, na kuongeza faida, akiendelea kufundisha wakulima wengine zaidi ya 650 wanaofuata nyayo zake. 

Rita Sekilovele, ni mnufaika mwingine ambaye alitumia ruzuku kutoka USAID kupanua biashara yake ya uzalishaji wa unga wa mahindi. 

Leo, kampuni yake, Super Seki, ni maarufu ikidhihirisha jinsi ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi unavyobadilisha maisha ya wanawake katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.

Sasa, jiulize mafanikio ambayo Tanzania ingeweza kupata kukiwa na masoko ya uhakika na washirika wengi wa ujasiriamali kama Prakseda na Rita. 

Kupitia USAID, Marekani imedhamiria kuhakikisha kwamba Watanzania wengi wanaweza kukuza biashara zao na kuwainua wengine. Ili kufikia lengo hili, tumeshirikiana tena na DFC kutoa dhamana za mikopo za ziada za dola milioni 52 kwa benki za Amana na CRDB. 

Hii itapanua kwa kiasi kikubwa mikopo katika sekta muhimu, ikiwa ni pamoja na uchumi katika sekta zisizo rasmi. 

Kati ya fedha hizi, dola milioni 34 zitalenga elimu na sekta isiyo rasmi, dola milioni 10 zitaelekezwa kwenye kilimo, biashara zinazomilikiwa na wanawake, na vijana, na dola milioni 8.8 zitaelekezwa katika sekta ya afya ili kuendeleza biashara na kukuza ushirikiano zaidi nchini Tanzania.

Ikiwa asilimia 75 ya idadi ya Watanzania wako chini ya umri wa miaka 35, na zaidi ya nusu ikiwa ni wanawake, mafanikio ya Tanzania yanategemea mafanikio ya vijana wake. 

Ndio maana tunawaweka vijana kuwa wa kipaumbele katika mipango yetu na ndio sababu tumedhamiria kupanua fursa kwa vijana wa Tanzania. Hivi karibuni USAID ilitoa ruzuku 160 kwa biashara za kilimo zinazoongozwa na vijana ili waweze kujipatia zana muhimu kama vile pampu za maji za jua, mashine za usindikaji chakula, na kivuli cha greenhouse. USAID pia ilitoa zaidi ya dola milioni 14 kwa biashara ndogo na za kati ili kukuza ajira.

Mipango hii inatarajiwa kuzalisha karibu dola milioni 43 katika mauzo mapya, ikiwamo asali na korosho kutoka Tanzania hadi nguo, na kutoa zaidi ya ajira 2,000 kwa Watanzania.

Mpango wa Sheria ya Marekani ya Ukuaji na Fursa wa Afrika (AGOA), ulioanzishwa mwaka 2000 na sasa unaotarajia kuendelezwa, unaziondolea biashara za Kitanzania ushuru wa kodi kwa bidhaa zinazouzwa nchini Marekani. 

Lengo la AGOA ni kutengeneza uhusiano wa biashara na mahusiano binafsi kati ya nchi zetu mbili kwa njia ambayo zote zinafaidika. 

USAID inafanya kazi na Wizara ya Viwanda na Biashara kupanua uelewa wa malengo ya AGOA na kusaidia kampuni zinazotaka kusafirisha bidhaa kwenda Marekani.

Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere, alisisitiza kwamba jamii yenye afya ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi. 

Kwa miongo kadhaa USAID, pamoja na mashirika mengine ya serikali ya Marekani, yamewekeza mabilioni ya dola katika kuimarisha mifumo ya afya nchini Tanzania. Kupitia ushirikiano na sekta binafsi, tumeanzisha suluhisho bunifu kutatua baadhi ya changamoto kuu.

Mpango huu umepunguza vifo vya kinamama na watoto wachanga kwa asilimia 25 katika maeneo yaliyolengwa. USAID inafanya kazi na sekta binafsi katika sekta zote, ili kufikia maslahi ya pamoja, kama vile kuwapa vijana wasio katika mfumo wa shule ujuzi wa ufundi na mafunzo katika sekta binafsi na umma, na hivyo kuwapa kizazi kijacho cha Watanzania zana na ujuzi ili wafanikiwe.

Ili biashara za Kitanzania zikue, zinahitaji mazingira salama na wezeshi ya biashara. Kuweza kuvuna faida za uwekezaji kunahitaji kuweka nia ya kukuza uwazi, maboresho ya mifumo ya masoko, uhuru wa kisiasa na kukabiliana na ufisadi. 

Ninapozungumza na kampuni za Kitanzania na kimataifa zinazovutiwa na kuwekeza nchini Tanzania, wanasisitiza umuhimu wa utawala bora, uwazi, na sheria inayofuatwa kwa usawa, ikiwa ni pamoja na sera za ushuru za haki na kuunda uwanja wa mashindano ulio sawa na wa haki. Mwisho wa siku, serikali zinazolinda haki za kisiasa na kiraia zinavutia mtiririko endelevu wa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje. USAID inafanya kazi pamoja na taasisi za Kitanzania ili kuweka mazingira rafiki ya biashara ambayo yanawawezesha kupanua biashara, kuwa na ubunifu na muhimu zaidi, kutengeneza ajira na fursa kwa vijana na wanawake wa Kitanzania. 

USAID imedhamiria kuimarisha ushirikiano huu sasa na kwa vizazi vijavyo, bega kwa bega na wajasiriamali kama Prakseda na Rita na mamilioni kama wao, ili kutafuta suluhisho zenye faida, haki, na endelevu kwa changamoto za maendeleo.