Mbaroni kwa kuuza mbegu za pamba za ruzuku gunia 30

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:08 PM Nov 26 2024
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari.
Picha: Marco Maduhu
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari.

JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga, linamshikilia Juma Peter Mtobela, kwa tuhuma za kuuza mbegu za pamba za ruzuku gunia 30 katika kijiji cha Maganzo wilayani Kishapu, kwa mtu ambaye hakufahamika na bado wanamtafuta.

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Amesema  Novemba 23 mwaka huu, katika kijiji cha Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, walimkamata Juma, kwa tuhuma za kuuza mbegu za ruzuku za pamba  gunia 30, kwa mtu ambaye alikimbia kusikojulikana na wanamtafuta.

Aidha, amesema jeshi hilo pia limewakamata wahamiaji haramu saba ambao ni Raia wa Burundi,katika kijiji cha Nyamilangano Halmashauri ya Ushetu Wilaya Kahama, kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria, na wamewapeleka katika ofisi za Uhamiaji kwa hatua zaidi za kisheria.

Amesema jeshi hilo pia, limewakamata watu 51 kwa tuhuma za wizi pamoja na vielelezo mbalimbali zikiwamo bangi kilo 10, pikipiki tisa, pombe aina ya moshi lita 15, godoro nne, kontena mbili za bati, mashine tatu za bonanza, gari likiwa na nondo 130, binding wire 11,mifuko 100 ya saruji, simu mbili, redio Saba, kabati,friji na kitanda kimoja. 

Amesema kwa upande wa kikosi cha usalama barabarani, limefanikiwa kukamata jumla ya makosa 7,920, ambapo makosa ya gari ni 5,615, bajaji na pikipiki ni 2,305, huku wakimfikisha mahakamani dereva mmoja kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja.

Katika hatua nyingine, Kamanda amesema Jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha usalama kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kesho (leo), na kutoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.