Ripoti za ugonjwa wa akili zaleta utata, kesi ya kuchoma mke

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 05:24 PM Nov 26 2024
Ripoti za ugonjwa wa akili  zaleta utata, kesi ya  kuchoma mke
Picha:Grace Gurisha
Ripoti za ugonjwa wa akili zaleta utata, kesi ya kuchoma mke

MFANYABIASHARA Khamis Luwongo (38) anayetuhumiwa kumuua mkewe Naomi Marijani na kisha kuuchoma moto mwili wake amedai kuwa ni aibu Hospitali ya Taifa ya Afya ya akili, Mirembe kupeleka mahakamani taarifa mbili tofauti zinazohusiana na akili yake.

Luwongo amedai hayo mbele ya Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya Daktari Bingwa wa Afya ya Akili, Sadiki Mandari kutoka Mirembe kukataa taarifa iliyotumwa mahakamani hapo ikiwa na jina lake na sahihi yake kwa madai kwamba haitambui.

Dk. Mandari amedai kuwa ripoti ya Septemba 26,2024 anayoitambua yeye ni hiyo aliyokwenda nayo yeye ambayo inaeleza kwamba siku ya tukio mshtakiwa alikuwa ana akili timamu,  lakini iliyotumwa na hospitali hiyo kuja mahakamani inayoeleza kuwa hakuwa timamu haitambui kwa sababu sahihi siyo yake.

"Ni aibu kwa taasisi inayoaminika na Serikali kutoa taarifa mbili kwa njia ya mtandao kuja mahakamani, daktari nae anakuja na yake anasema ya kwake ndiyo bora zaidi, amekuja kutia aibu taasisi hofu yangu ni kuletewa ripoti mbili ya Mkeamia,"

"Hii wameleta ripoti mbili, hawakawii hawa mawakili wa Serikali kuleta ripoti ya pili ya Mkemia na kusema haya majivu ni ya Naomi,"alidai Mshtakiwa Luwongo 

Hata hivyo, Jaji Mwanga alimtoa hofu nakumueleza kwamba yeye ndiye anayejua kama ana husika au la, kwa hiyo mahakama itatoa uamuzi.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama hiyo imepokea ripoti mbili kuhusiana na uchunguzi wa akili ya mshtakiwa Luwongo kama vielelezo katika kesi hiyo.

Mshtakiwa Luwonga ambaye ni Mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa Mei 15, 2019 akiwa Gezaulole eneo la Kigamboni alimuua Naomi Marijani.