CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimesema kukua kwa teknolojia hususan matumizi ya mitandao ya kijamii, kumeongeza kasi ya udhalilishaji wanawake na wasichana mitandaoni.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben, amesema bado kuna changamoto zinazoibuka zikichagizwa na sheria mbalimbali, ambazo zina mapengo na kukuza ukatili wa kijinsia kutokana na maendeleo ya teknolojia.
“Matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, yameathiri jamii hasa wanawake na wasichana ambao ndio mara nyingi wamekuwa walengwa wa picha zinazowadhalilisha,” ameeleza.
“Kuna ongezeko kubwa la unyanyasaji wa kijinsia, kwa njia ya mitandao ya kijamii. Tunaungana na Watanzania, kukemea vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na wasichana, hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Dk. Rose, amesema hayo, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, zinazolenga kuimbusha jamii kuachana na matendo ya ukatili, kama vile vipigo, ukeketaji, ubakaji, ulawiti, mimba za utotoni na rushwa ya ngono.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED