Kairuki yaja na teknolojia kutibu saratani bila upasuaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:33 PM Nov 25 2024
Wauguzi wa hospitali ya Kairuki Mikocheni  wakiwa wanawaandaa wagonjwa kwenye mtambo wa HIFU unaotibu saratani bila upasuaji ambao ni wa kwanza Afrika Mashariki na Kati.
Picha:Mpigapicha Wetu
Wauguzi wa hospitali ya Kairuki Mikocheni wakiwa wanawaandaa wagonjwa kwenye mtambo wa HIFU unaotibu saratani bila upasuaji ambao ni wa kwanza Afrika Mashariki na Kati.

Dk Fredy Rutachunzibwa kutoka Hospitali ya Kairuki ni Mtanzania wa kwanza kufuzu mafunzo ya kutibu saratani kwa kutumia teknolojia ya HIFU (High-Intensity Focused Ultrasound), ameeleza namna tiba hiyo inavyotolewa bila upasuaji.

 HIFU ni teknolojia ya kisasa inayotumia mawimbi ya sauti yenye nguvu kuteketeza seli za saratani kwa usahihi, bila kuhitaji upasuaji. 

Akizungumza na Nipashe Digital, daktari huyo amesema mbinu hiyo inapunguza maumivu, hatari ya maambukizi na muda wa kupona kwa wagonjwa. 

Amesema Hospitali ya Kairuki ni ya kwanza Tanzania, Afrika Mashariki na Kati kutumia teknolojia ya HIFU, na ni ya tatu Barani Afrika. 

Amesema teknolojia hiyo inatoa suluhisho kwa wagonjwa wengi wa saratani, hasa wale wanaokosa matibabu ya kisasa kutokana na vikwazo vya kifedha au umbali wa hospitali.

Dk Rutachunzibwa ambaye alipata mafunzo hayo nchini China mwaka jana amesema matibabu kwa kutumia HIFU hayaingizi chochote ndani ya mwili.

Wauguzi wa hospitali ya Kairuki Mikocheni wakiwa wanawaandaa wagonjwa kwenye mtambo wa HIFU unaotibu saratani bila upasuaji ambao ni wa kwanza Afrika Mashariki na Kati.
“Ngozi haiguswi na hakuna kidonda kinachotengenezwa, hakuna nusu kaputi yaani mgonjwa anaondolewa uvimbe huku akiwasiliana na daktari anayemhudumia,”amesema na kuongeza; 

“Kinachofanyika ni kwamba mawimbi sauti yanapelekwa katika eneo lenye uvimbe unaunguzwa bila kuathiri sehemu zingine na matibabu haya yanatolewa kwa wenye saratani za aina mbalimbali,” amesema

 Amesema HIFU inaboresha huduma za afya kwa kuongeza ufikiaji wa matibabu ya kisasa na kupunguza vifo vinavyosababishwa na saratani nchini Tanzania.

 “ Teknolojia hii ni hatua muhimu katika mapinduzi ya sekta ya afya nchini kwasababu matibabu haya walilazimika kuyafuata mataifa yaliyoendelea lakini sasa ayanapatikana hospitali ya Kairuki,” amesema.