Kesi watumishi 15 wa jiji ngoma nzito

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 10:10 AM Nov 25 2024
Mahakama
Mtandao
Mahakama

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi, imekataa kupokea kielelezo cha flash yenye taarifa za miamala ya fedha za Manispaa ya Ilala kutokana na shahidi kushindwa kueleza kilichomo ndani yake.

Uamuzi huo wa mahakama umetolewa mbele ya Jaji Sedikia Kisanya wakati shahidi wa tano wa upande wa mashtaka Edgar Paul akitoa ushahidi katika kesi ya kulisababishia jiji hasara ya Sh. bilioni 8.9 inayowakabili watumishi 15.

Washtakiwa katika shauri hilo ni Tulusubya Kamalamo na wenzake 14 wanaokabiliwa na mashtaka 142, yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya ofisi na kusababishia jiji hasara ya Sh. bilioni 8.9.

Edgar katika ushahidi wake alidai ni ofisa kutoka Benki ya CRDB na miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha mfumo wa benki unafanya kazi ipasavyo.

Alidai kuwa Machi 12, 2023, akiwa ofisini, alitakiwa kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhusu miamala ya fedha katika akaunti ya Manispaa ya Ilala kuanzia Januari 2019 hadi Desemba 2021.

"Niliingia katika mfumo wa benki kuchukua taarifa hizo, nilikuta ziko kurasa 10,000, tukaamua kutoa kurasa 10 za mwanzo na kurasa 10 za mwisho kisha taarifa yote ya miamala hiyo nikaingiza katika flash," alidai.

Shahidi aliomba kifaa hicho kipokewe mahakamani kama kielelezo cha upande wa mashtaka.

Upande wa utetezi ulipinga kupokewa kwa kielelezo hicho kwa kuwasilisha hoja mbalimbali.

Wakili Constantine Kakula alidai flash isipokewe kwa sababu shahidi alishindwa kuweka msingi muhimu kwa 

kuelezea flash na taarifa zilizomo ndani yake.

Alidai shahidi hakueleza anakitambuaje kilichomo ndani ya flash ili atakaporuhusiwa kufungua flash hiyo alichokielezea kikutwe ndani yake.

Hoja nyingine ya upande wa utetezi ni kwamba watuhumiwa hawakupewa nafasi ya kuangalia flash kama kanuni inavyotaka na kwamba wakati wa kusomewa maelezo ya mashahidi, haikutajwa.

Upande wa Jamhuri ulidai wakati washtakiwa wanasomewa maelezo ya mashahidi, flash yenye miamala ya fedha za Manispaa ya Ilala ilisomwa, hivyo hoja hiyo haina mashiko.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama ilipokea flash kwa ajili ya utambuzi na kukataa kupokewa kama kielelezo cha upande wa mashtaka.

"Shahidi aliomba mahakama kukubali flash yenye taarifa ya benki bila kubainisha vilivyomo ndani yake. Kulingana na hali ilivyo, mahakama inaona kwamba shahidi alishindwa kuonesha flash disk na taarifa zilizomo ndani yake kama inavyotakiwa na sheria.

"Kwa tukio hili, ninaunga mkono hoja ya pingamizi flash inayoombwa kupokewa kama kielelezo, hairuhusiwi kupokewa," alisema Jaji Kisanya.

Mahakama hiyo ilikubaliana na hoja moja ya Wakili Kakula kwamba shahidi alishindwa kuelezea kilichomo ndani ya flash.

Washtakiwa katika shauri hilo wanadaiwa kati ya mwaka 2019 na mwaka 2021, waliongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka kwa kushindwa kuingiza mapato ya Halmashauri ya Jiji yanayotokana na vyanzo mbalimbali vya mapato katika akaunti za CRDB, NMB, NBC na DCB na hivyo kujipatia manufaa ya Sh. bilioni 8.9.

Pia wanadaiwa kulisababishia Jiji la Ilala hasara ya kiasi hicho cha fedha. Shauri hilo linaendelea leo.