HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia kuanza kutoa tiba ya upandikizaji ini mwakani kutokana na kuwapo mahitaji hayo, hasa kwa wagonjwa wanaohudhuria kliniki ya ini hospitalini huko.
Uongozi wa hospitali hiyo ya hadhi ya juu zaidi nchini umesema kuwa zaidi ya wagonjwa 5,000 wana tatizo la ini na kati yao, 2,333 wana uvimbe kwenye ini huku 607 wakigungulika kuwa na saratani ya ini na kusinyaaa kwa ini, hivyo wakihitaji huduma ya kupandikizwa ini.
Mkurugenzi Mtendaji MNH, Prof. Mohamed Janabi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa kwa mwaka mmoja na nusu, hospitali hiyo imekuwa inafanya maandalizi ya kuanzisha huduma hiyo kwa kushirikiana na matabibu wenzao wa India.
"Kwa hizi siku mbili (mwishoni mwa wiki), tumefanya uchunguzi kwenye OPD (wagonjwa wa nje) na watu wapatao 100 tumewaona, na miongoni mwao tumewakuta wana tatizo. Huu ni mchakato wa kujijengea uwezo, tunahitaji wauguzi, wataalamu wazuri eneo hili.
"Wenzetu wa India wameanza upandikizaji ini tangu mwaka 2002. Kupitia Idara ya Mfumo wa Chakula (ya MNH), walikuwa na wenzetu kutoka India ili mwakani tuanze huduma hii. Tulitaka kujua kwanza wagonjwa wangapi wana tatizo, tumewaona zaidi ya 100. Tunahitaji wataalamu wa usingizi, madaktari, yaani tuwe na seti ya eneo hili," alisema Prof. Janabi.
Alisema kusogeza huduma hizo karibu na wananchi, kutapunguza gharama nyingi za kupeleka wagonjwa hao kutibiwa nje ya nchi. Alisema huduma hizo hazikuwapo nchini kutokana na kukosa utaalamu, vifaa vya uchunguzi au miundombinu stahiki ya kutolea huduma hizo.
"Tumeshirikiana na wataalamu kutoka Hospitali ya Fortis ya India, ambao wamekuwa na madaktari wetu kwa siku tatu, wameona wagonjwa mbalimbali wa magonjwa ya ini na kufanya tathmini ya hali ya upatikanaji dawa, miundombinu ya maabara, ICU (chumba cha uangalizi maalumu) ambayo inakidhi mahitaji ya huduma hiyo," alisema.
Jenifer Choudhary, Mkurugenzi wa Biashara kutoka Vaidam Health ya India, alisema ni furaha kupata fursa ya kufika nchini kwa ajili ya kufanya maandalizi ya huduma hiyo.
"Huduma hii inahitaji kufanya maandalizi na si kufanyika kwa awamu moja pekee na wakati huu tumefika kufanya maandalizi ya awali na kuwafanyia uchunguzi wagonjwa na mahitaji yatakayohitajika ili kufanikisha awamu ya pili.
"Tuna matumaini huduma hii itafanyika kwa uhalisia, lakini awamu za maandalizi zinaweza kufikia tatu kabla ya kuanza upandikizaji kwa wagonjwa," alisema Choudhary.
Dk. Gaurav Gupta kutoka Hospitali ya Fortis ya India, alisema upandikizaji ini ni safari inayohitaji maandalizi na itafanikiwa kutokana na kuwapo vifaa na wataalamu.
Bingwa Mbobezi wa Upasuaji wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini na Bingwa wa Upasuaji kupitia Tundu Dogo MNH, Dk. Kitembo Salumu alisema kuwa hadi sasa takwimu za hospitali zinaonesha kuna zaidi ya wagonjwa 5,000 wenye shida katika ini.
Alisema kuwa kati yao, 2,333 wana uvimbe kwenye ini na 607 wamegungulika kuwa na tatizo la saratani ya ini, wengine ini kusinyaa na hivyo kuhitaji huduma ya kupandikizwa ini.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED