MWANAFUNZI wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mogabiri, wilayani Tarime, mkoani Mara, Julius Nchagwa anadaiwa kufariki dunia baada ya kuanguka katika uwanja wa shule hiyo muda mfupi baada ya kutoka katika chumba cha mtihani.
Ndugu wa mtahiniwa huyo wamegoma kuchukua mwili wake, wakishinikiza uchunguzi kuhusu chanzo cha kifo chake, wakidai miezi kadhaa nyuma alikuwa na ugomvi na uongozi wa shule hiyo.
Mzazi wa mwanafunzi huyo, Daniel Marwa, mkazi wa kijiji cha Nyabitocho, wilayani hapa, alisema hawako tayari kuchukua mwili wa kijana wao kwa kuwa kuna utata juu ya chanzo cha kifo chake.
Alisema hofu ya familia inatokana na madai kwamba miezi kadhaa iliyopita, kijana wao alikuwa na ugomvi na uongozi wa shule hiyo, hali iliyosababisha kusimamishwa masomo na uongozi wa shule.
"Wanafamilia tumeshauriana kwanza tusichukue mwili wa marehemu hadi taratibu zote za uchunguzi zitakapofanyika kwa kuwa kifo cha kijana wetu kina utata kutokana na kuwapo ugomvi baina yake na uongozi wa shule hapo awali," alidai.
Mashuhuda wa tukio hilo walidai mtahiniwa huyo alikuwa anatetemeka, hata kuanguka kwenye uwanja wa mpira na kupoteza fahamu. Inadaiwa alifariki dunia kabla ya kupata huduma za kitabibu.
Mmoja wa wanafunzi shuleni huko, Ng'anga Thomas alidai kuwa yeye na wenzake waliitwa kutoa msaada kwa mtahiniwa akiwa ameanguka kwenye uwanja wa mpira, mita chache kutoka madarasa ya shule hiyo.
"Tulifika eneo hilo na kumkuta akiwa anatetemeka na kuonesha dalili za ajabu ambazo hatukuzielewa wakati huo, tukambeba kumpeleka hospitalini ambako hata hivyo tuliambiwa baadaye alikuwa ameshafariki dunia," alidai mwanafunzi huyo.
Mkuu wa Shule hiyo, Magudila Mgeta alisema mwanafunzi huyo alifanya makosa ya utovu wa nidhamu miezi kadhaa iliyopita ikiwamo kumpiga mwanafunzi mwenzake na kukataa kutii maagizo halali ya walimu.
"Alipelekwa katika Kamati ya Nidhamu, nako pia akakaidi, hatimaye Bodi ya Shule ikaamuru asimamishwe shule, lakini arejee kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, alirejea baadaye shuleni na kuruhusiwa," alisema.
Mwalimu huyo alisema juhudi za kuokoa maisha ya mtahiniwa huyo hazikufanikiwa kwa kuwa alifariki dunia kabla ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mji wa Tarime.
Alisema vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na madaktari ili kuja na maelezo kamili kuhusiana na chanzo cha kifo hicho na kuwa ripoti itakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED