Mbowe: CHADEMA ni mpango wa Mungu, CCM watambia 4R

By Elizabeth Zaya ,, Romana Mallya , Nipashe
Published at 12:14 PM Nov 25 2024
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Picha: CHADEMA
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

KAMPENI za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zinaendelea.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema chama hicho ni "mpango wa Mungu" ndiyo maana licha ya vikwazo vingi kimeendelea kuwa imara.

Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umewafilisi hoja zote wapinzani kwa sababu yote yaliyokuwa yanapigiwa kelele ameyatekeleza.

Chama hicho kinachoongoza serikali kimesema Falsafa ya 4R (Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu), Reform (Mabadiliko) na Rebuiding (Kujenga upya) ya Rais Samia ni mtaji mkubwa kwao.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla, aliyasema hayo jana wakati wa kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Kata ya Kivule, Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam, ikiwa ni siku ya tano ya kampeni mkoani humo.

"Wamekubali kuwa muziki huu CCM wanayo haki kupita kwa kishindo. Siasa si ugomvi. Na huyu wa Chama cha TLP (Mwenyekiti wa TLP, Aivan Maganza) ameona namna serikali  na uongozi wa Rais Samia kazi alizofanya.

"Kwa kweli Rais Samia amewafilisi hoja zote wapinzani, yote yaliyokuwa yakipigiwa kelele ameyafanyia kazi," alitamba Makalla ambaye pia ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

Makalla alisema yanayoendelea mikoani, kwa lugha nyepesi kwa CCM ni kwamba 'yajayo yanafurahisha' akifafanua kuwa ushindi wa kishindo kwa chama tawala unakuja.

Aliwaomba wananchi wawachague wasaidizi wazuri wa mitaa kutoka chama tawala kwa kuwa mafanikio yote ni ushirikiano kati ya viongozi wa chini hadi ngazi ya Rais.

'MPANGO WA MUNGU'

Wakati CCM wakitamba na 4R, Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe, amesema kuwa baada ya chama hicho kupita katika kile anachokiita "bonde la uvuli wa umauti" kwa miaka saba, wamejipanga kurejesha heshima yao.

Mbowe alitoa kauli hiyo wakati akihutubia wananchi wa Kyela, mkoani Mbeya wakati akiwanadi wagombea wa nafasi mbalimbali kupitia chama hicho kwenye kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Alisema kuwa pamoja na chama hicho kupitia katika mawimbi mengi, kimeendelea kusimamia na kuwa chama kikuu cha upinzani kwa sababu ni mpango wa Mungu kuwapo.

"Chama chetu ni imara, kimepigwa mawimbi mengi, lakini kwa kuwa ni mpango wa Mungu hakiwezi kufa kwa sababu ya visa. Kipindi cha miaka saba, kuna wengine hatukufa 'mazee...' lakini cha mtema kuni tulikipata. Sasa tumevuka bonde la uvuli wa umauti, tusiendelee kulalamika, tujipange kwenda mbele na hakuna kukata tamaa, kesho yetu iliyo bora zaidi inakuja.

“Tunapokwenda kwenye uchaguzi huu, tunaanza tena kurejesha heshima ya CHADEMA iliyoporwa kwa kukamata vitongoji, vijiji na mitaa, kikaongoze misingi huku chini," alisema.

Mbowe alisema chama chao kimejengwa kwa gharama kubwa, ikiwamo kwa kupitia dhoruba mbalimbali ambazo hata hivyo hawakukata tamaa kukipigania.

Mbowe alisisitiza kuwa hata kama chama hicho kikishika madaraka, licha ya kupitia vipindi vigumu vya ujenzi wa demokrasia, hakitakuwa tayari kuwa na visasi.

"Ujenzi wa demokrasia ya nchi hii kwa zaidi ya miaka 30, unataka kuchagua viongozi wanaoaminiwa na watu, CHADEMA siku tutakapokamata madaraka, hatutafanya kisasi, kisasi ni kazi ya Mungu, tutasimamia haki kwa sababu taifa lisilo na haki haliwezi kuwa na baraka za Mungu," alisema Mbowe.

Alisema chama hicho kimejengwa kwa misingi mikuu minne; haki, uhuru wa watu, kuamini katika demokrasia na maendeleo ya watu, hivyo kitaendelea kuisimamia kikishika madaraka.

"Ukisema wewe ni mwana-CHADEMA, usiangalie sura ya Mbowe, tafakari misingi hiyo inayounda chama hiki, tangu kimeasisiwa, kimepambana na mawimbi yote kwa sababu kina imani na si maigizo, ninaomba imani hii ndiyo iwaimarishe," alisema.

ACT WAZALENDO

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendio, Ado Shaibu, akiwanadi wagombea wa chama chake katika kijiji cha Kajima, kata ya Kajika, jimboni Tunduru, alisema safari hii wamejipanga kudhibiti alichokiita "uporaji" katika uchaguzi huo.

"Sisi tumevumilia sana kuibiwa, mwaka 2020 tuliibiwa, na safari hii wamejaribu kutubipu tumewapigia, pengine huko walipo wanajipanga eti wajaribu kutuibia tena, ninawaambia simu zetu tumeweka bando la kifurushi cha mwaka, ataumia mtu safari hii, sisi tumejiandaa, tumejipanga, tusikubali haki yetu ya kuongoza kijiji iporwe," alisema Ado.

TAMKO LA RAIS

Kupitia tamko lake la Novemba 22 mwaka huu lililotangazwa rasmi jana, Rais Samia ametangaza tarehe 27, 2024 kuwa siku ya mapumziko kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, tamko hilo limetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa, Sura 35, kinachompa Rais mamlaka ya kutangaza siku yoyote kuwa ya mapumziko kama nyongeza ya siku zilizoainishwa kwenye jedwali la sheria hiyo au kubadili siku yoyote kati ya zilizoainishwa na siku hiyo kuwa ya mapumziko kama vile imetajwa kwenye jedwali la sheria.

"Na kwa kuwa tarehe 27 Novemba 2024, Jumatano, ambayo ni siku ya kazi, imetangazwa na waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa kuwa siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024, Rais anakusudia kutangaza Siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwa siku ya mapumziko," inasomeka sehemu ya tangazo hilo lililotolewa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI jana.