Samia: Dini ni sehemu pekee kujenga jamii yenye maadili

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 11:18 AM Nov 26 2024
Rais Samia Suluhu Hassan

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa dini zina sehemu muhimu na ya kipekee katika kuendelea kujenga jamii yenye maadili, umoja, upendo, amani na mshikamano.

Pia amewakumbusha waumini wa dini ya Kiislam kuendelea kujenga madrasa nyingi zaidi, ili kuwapatia watoto mafunzo ya kiimani yatakayowawezesha kuwa raia wema na waadilifu kwa familia na taifa kwa ujumla.

Amewataka waumini wa madhehebu ya dini kutumia nyumba za ibada kujijenga kiimani badala ya kuzitumia kama chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani.

Rais Samia alisema hayo mjini Morogoro baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Msikiti wa Al Ghaith unaotajwa kuwa mkubwa wa kwanza kwa Afrika Mashariki ulio chini ya Taasisi ya Islam Foundation unaofadhiliwa na Jumuiya ya Dar al ber Society ya Dubai kutoka nchi ya Falme za Kiarabu na ukikamilika utagharimu shilingi bilioni saba.

"Ni vyema nyumba hizi za ibada zikatumika kuunganisha kamba ya waumini na sio kukata kamba hiyo inayounganishwa na Mungu, mkajiita ni viongozi wa dini wakati huo huo mnasababisha mifarakano kwa waumini wenu, msifike huko mjue binadamu huwa wanatofautiana," alisema Rais Samia.

Aidha, alisema katika maeneo mengine nyumba za ibada zinazojengwa badala ya kuleta neema na kuwafanya waumini kuabudu na kupata heri kwa pamoja wengine wamekuwa wakizigeuza chanzo cha vurugu.

Katika hatua nyingine, Rais Samia akitumia kusanyiko hilo kuwafunda wanawake kwenye jukumu la malezi kwa watoto ili kupunguza ama kumaliza changamoto ya mmomonyoko wa maadili unaoendelea badala ya jukumu hilo kuwaachia wanaume.

Aidha, aliwaasa kinamama kutenga muda wa kutosha kwa ajili ya malezi ya watoto badala ya kutegemea kinababa ambao ndio wamekuwa wakiogopwa na watoto kwa sasa kwa kuwa mtoto anapokosea badala ya mama kukaa naye chini na kumfundisha humtishia kuyafikisha kwa baba yake.

"Mama anamwambia mtoto kila nikikwambia husikii sasa ngoja baba ako aje, kwa nini umtishie baba na kwanini wewe mama usisimame kama wewe kwa kutumia lugha nzuri na kumwelewesha mtoto na akakuelewa? Kinamama mkaze kamba katika suala zima la malezi yanayofaa ambayo yanakwenda sambamba na imani kwa kusimamia misingi ya malezi bora kwa watoto wenu," alisisitiza Samia.

Pamoja na kupongeza Taasisi ya Islamic Foundation kujenga misikiti zaidi ya 1,000 nchini, aliwahimiza ujenzi wa madrasa za kutosha ili zisaidie kutoa elimu kwa watoto na kuwa na jamii yenye maadili mema na kumjua Mungu.

Aliipongeza taasisi hiyo pia kuendelea kutoa michango yake kwenye jamii hususani kwenye sekta za afya, elimu na maji na kwamba hatua hiyo ni sadaka nzuri inayoishi wakati wote kwa kuwa huduma hizo ni muhimu kwenye jamii.

Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni, alimpongeza Rais Samia kwa kuwa mstari wa mbele kushiriki matukio anayoalikwa na taasisi za dini. 

Alisema pamoja na serikali kusimamia vyombo vya ulinzi na usalama katika suala zima la kulinda amani na utulivu, taasisi hizo za dini zina mchango mkubwa katika kulinda amani na utulivu.

"Lakini baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia kipindi hiki cha uchaguzi kushawishi wananchi kujiingiza katika vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani ni vyema mkajiepusha na hali hiyo ili kuendelea kufaidi matunda ya amani na utulivu uliopo," alisema Waziri Masauni.

Naye Rais wa Taasisi ya Islamic Foundation, Arif Nahad, alisema mradi huo wa msikiti ulianza kujengwa Oktoba, 2021 na sasa umefikia asilimia 80 ya utekelezaji ambao ukikamilika utawezesha kuwapokea waumini 3,000 kwa wakati mmoja na huduma nyingine kama eneo la kuhifadhia na kuosha maiti, maktaba ya kisasa, nyumba za kupumzikia mashehe pamoja na madrasa.

"Taasisi hii imefanikiwa kujenga misikiti zaidi ya 1,600 katika maeneo mbalimbali kwa Tanzania Bara na Visiwani na misikiti hiyo ina madrasa zenye wanafunzi takribani 80,000.

“Tumekuwa pia tunatoa huduma ya majisafi na salama kwa jamii kwa kuchimba visima virefu na vifupi ambapo kwa sasa tumefanikiwa kuchimba visima zaidi ya 3,000 kwenye maeneo mbalimbali Tanzania bara na visiwani," alisema Nahad.

Alimwomba Rais Samia kuisaidia taasisi hiyo kufanikisha ujenzi wa chuo cha ualimu na maadili katika eneo lake lenye ekari zaidi ya 38 lililoko Kitungwa wilayani Morogoro, ombi ambalo Rais aliliridhia.

Rais Samia amemaliza ziara yake ya siku mbili mkoani Morogoro na kuelekea mkoani Dodoma.