MATUMAINI ya ubingwa kwa timu ya KMKM SC yameendelea kuingia doa baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Mlandege FC katika mchezo wa 12 wa Ligi Kuu Zanzibar.
Mchezo huo uliovuta mashabiki wengi uwanjani ulichezwa juzi, Jumapili katika dimba la Mau A majira ya saa kumi za alasiri.
KMKM imeendelea kupata matokeo mabaya karibu michezo minne mfululizo jambo ambalo mashabiki wake wameanza kupoteza matumaini ya mbio za ubingwa msimu huu ingawa bado ni mapema.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Kocha wa KMKM, Ame Msimu, alisema mchezo huo ulikuwa mgumu katika dakika zote 90.
Alisema tangu hapo awali alicheza kwa kujihami na kujilinda zaidi kwa kuwa aliwafahamu wapinzani wao wana wachezaji machachari.
Alisema timu yake ilicheza vizuri, lakini makosa madogo ya safu yake ya ulinzi ndiyo yaliyowapa wapinzani wao bao la pili.
Alisema bao la pili lilitokana na mpira uliopigwa nje ya boksi na kutinga moja kwa moja wavuni jambo ambalo wachezaji wake wangekuwa makini na mpigaji wa mpira huo wangefanikiwa kuzuia shambulizi hilo.
“Tulicheza na timu ambayo ina wachezaji machachari na hodari, kuna wakati tulikosa umakini kutokana na kasi ya mchezo jinsi ulivyokuwa, lakini bahati ilikuwa yao wametufunga,” alisema.
Aidha, alisema bado ni mapema kwa mashabiki wa timu hiyo kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa kwani wanayo nafasi ya kurekebisha makosa yaliyopo na timu ikarudi kufanya vizuri.
Kwa matokeo hayo Mlandege FC imekwea kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha alama 24, nafasi ya pili ikishikiliwa na mafunzo yenye alama 23 ambayo bado hajacheza mchezo wake wa 12.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED