JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya, linawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni Ramadhan Mwakilasa (28) na Mariamu Mwashambwa (28), wakazi wa TEKU viwandani Jijini Mbeya, kwa tuhuma za mauaji ya mtoto Chloy Ramadhan (04) kwa kumpiga fimbo sehemu mbalimbali za mwili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (SACP) Benjamini Kuzaga, amethibitisha kukamatwa watuhimiwa hao, Novemba 25, 2024.
Amesema mtoto Chloy alifariki dunia baada ya kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi aitwaye Mwakilasa akishirikiana na mama yake wa kambo aitwaye Mariamu.
“Uchunguzi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ukatili na unyanyasaji kwa kumuadhibu mtoto baada ya kujisaidia kwenye nguo alizokuwa amezivaa,” amesema Kamanda Kuzaga.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Kuzaga, linawataka wazazi/walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watoto pindi wanapokosea na badala yake watumie njia sahihi na salama kuwafundisha au kuwaelekeza bila kusababisha madhara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED