Tumefunguliwa macho elimu ya mpiga kura

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 04:34 PM Nov 26 2024
Wananchi wa kwa Sadala, Wialaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wakisikiliza elimu ya mpiga kura inayotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la TUSONGE CDO kwa kushirikiana na Taasisi ya WAJIBU.
Picha: Godfrey Mushi
Wananchi wa kwa Sadala, Wialaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wakisikiliza elimu ya mpiga kura inayotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la TUSONGE CDO kwa kushirikiana na Taasisi ya WAJIBU.

WAKATI vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji vikihitimisha kampeni zake leo, kupisha uchaguzi wa viongozi hao Novemba 27, wananchi wa kwa Sadala, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wameeleza kufurahishwa kwao na namna walivyojengewa uwezo na ujasiri wa kushughulika na viongozi wasiowajibika.

Katika mkutano wa utoaji elimu ya mpiga kura, uliofanywa leo na Shirika lisilo la kiserikali la TUSONGE CDO, baadhi ya wakazi wa kwa Sadala wamesema hamasa hiyo imewafungua macho.

Mfanyabiashara wa Soko la Kwa Sadala, Allan Masacky, amesema elimu hiyo imewasaidia kujua ni kwa namna gani watamalizana na wagombea wenye uchu wa madaraka na wanaotafuta uongozi kwa njia ya rushwa.

“Hii hamasa inayofanywa na TUSONGE kuwaamsha wananchi kuchagua viongozi bora na kushiriki mikutano ya kampeni ni nzuri, kwa sababu hatuwezi kuchagua viongozi mzigo wala wala rushwa wanaoshawishi wananchi kuwachagua kwa kuwapa fedha. 

“Elimu tuliyoipata hapa ni namna bora ya kuwapata viongozi wa kidemokrasia, wanaotamani kuwajibika kwa ajili ya wananchi na watu wenye uadilifu katika jamii.” 

Wakati, Gloria Tarimo, mfanyabiashara ya ndizi, amesema elimu ya kushiriki kupiga kura kumchagua kiongozi bora anayemtaka, liko jambo kubwa alilojifunza, kwamba ni haki ya kila Mtanzania kupiga kura kumchagua yule ambaye anafaa na anayeweza kuwavusha katika gurudumu la maendeleo kwenye kijiji chao.

“Tumejifunza tunapaswa kuchagua mtu anayeweza kutatua changamaoto zetu na kusikiliza wananchi wake wasema nini.Hatutachagua mtu ambaye anatumia nguvu ya fedha kuingia madarakani. Huyo ni lazima tujiulize kuna nini mpaka ananunua madaraka.”