IKIWA imebaki siku moja kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini, Mgombea wa Chama cha ACT Wazalendo katika kijijii cha Igung'wa kata ya Kitwana wilayani Kahama mkoani Shinyaga, William Nkwabii ameandika barua ya kujitoa katika nafasi hiyo na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akiongea na Nipashe Digital leo, Nkwabi amesema,ameamua kuandika barua hiyo baada ya daktari kumpima na kubaini kuwa anatakiwa kupumzisha mwili wake kutokana na umri alionao kwa sasa kushindwa kufanya kampeni.
Nkwabia amesema,amefikia maamuzi hayo bila kushawishiwa na mtu huku akiwa na akili timamu na kwamba kwa sasa atakuwa mwananchi wa kawaida katika kijiji hicho na atashiriki kuchaguzi viongozi na wajumbe wa serikali ya kijiji kama walivyo wengine.
Aidha amesema, kwasasa atamuunga mkono mgombea wa CCM na kuwaomba waliokuwa wafuasi wake kutoka ACT Wazalendo kuungana naye katika kumuunga mkono mgombea huyo.
"Kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo nilikuwa CCM na sasa narudi nyumbani ili kuungana na wenzangu kama ilivyokuwa hapo awali na nitamchagua kiongozi anayetokana na chama hiki. Niwaombe wafuasi wangu tuliokuwa pamoja tukiunge mkono Chama cha Mapinduzi" amesema Nkwambi.
Awali akimpokea Nkwabia, Mwenyekiti wa CCM kata ya Maalunga, Baraka Jilumbi amesema, mlango wa chama chao huko wazi kwa mtu yeyote anayetaka kujiunga na chama hicho na hiyo ndio sababu Nkwambi amejitoa na kuunga juhudi.
Hata hivyo Jilumbi amesema, kwa kazi anazozifanya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan haoni sababu ya mwananchi yeyote kuendelea kubaki katika vyama vingine na badala yake waungane kwa pamoja katika kufikisha maendeleo kwa wananchi hasa katika sekta ya afya, maji, miundombinu ya barabara na kilimo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED