WAZIRI wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, ametoa angalizo kwamba kifungu kilichotumika katika kesi ya umri wa kuoa na kuolewa iliyofunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, hakikuwa sahihi.
Prof. Kabudi alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam wakati akifungua kampeni ya siku 16 za uanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia iliyojumuisha wadau wa Mtandao wa Kupinga Ukatili (MKUKI) chini ya uratibu wa Shirika la Wanawake na Maendeleo Afrika (WiLDAF).
"Lakini niseme, kwa sisi wanasheria wa Tanzania tumeanza kusahau mfumo wetu wa sheria, sisi tunatumia The English Common Law System. Uamuzi wa mahakama ni sehemu ya sheria zetu, hasa ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
"Lakini makosa hayo si yenu, makosa hayo ni ya sisi wasomi, sisi wanataaluma, hatujaandika ‘commentary’ ya Katiba yetu kama walivyofanya wenzetu wa India, ndio maana kila mtu anapoisoma Katiba anaisoma ilivyo. Inabidi tuandike ‘commentary’ ya Katiba, kwamba kila kwenye kifungu cha Katiba tuweke uamuzi wa mahakama.
"Na ndio maana ile kesi ya Gyumi... mimi kwa maoni yangu, kifungu kilichotumika hakikuwa sahihi, ningekuwa mimi, nisingetumia ibara ya 13 na nilisema bungeni watu hawakunielewa," alisema Prof. Kabudi.
Gyumi alifungua shauri Mahakama Kuu ya Tanzania kwa niaba ya watoto wote walio katika hatari ya kuingia katika ndoa za utotoni dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2016, kupinga uhalali wa kikatiba wa ndoa za utotoni.
Rebecca alishinda shauri hilo baada ya mahakama hiyo kutamka kwamba vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ni vya kibaguzi na vinakwenda kinyume cha Katiba na kwamba vimepitwa na wakati.
Alipinga vifungu hivyo vya 13 na 17 kwa msingi kwamba vinakiuka ibara ya 12(1) ya Katiba ya Tanzania inayotoa usawa kwa watu wote.
Pia alipinga kwamba vifungu hivyo vinakiuka ibara ya 13(1) na (2) vya Katiba hiyo ya nchi ambayo inawalinda watu dhidi ya ubaguzi kwa misingi ya kijinsia.
Alidai vifungu hivyo vya sheria pia vinakiuka ibara ya 21(2) ya Katiba hiyo kwa kutowapa wasichana fursa ya kushiriki kikamilifu katika kuamua mustakabali wa maisha yao na kwamba vinamnyima mtoto haki ya kupata elimu na uhuru wa mawazo.
HUKUMU YA KESI
Mahakama Kuu Julai 8, 2016, ilitoa hukumu ikitamka kuwa, ndoa yoyote ya mtu mwenye umri chini ya miaka 18 ni kinyume cha sheria na kwamba vifungu hivyo vinaruhusu watoto kuingia katika ndoa wakati haifai kuwaingiza watoto katika majukumu makubwa ya ndoa na kuonesha hatari zake kiafya inayowakabili watoto hao pale wanapoolewa wakiwa na umri mdogo.
Mahakama ilitoa uamuzi kwamba vifungu hivyo havitoi usawa kwa msichana na mvulana katika njia mbili; kwanza umri wa ndoa tofauti kati yao na pili, wasichana chini ya umri wa miaka 18 wanahitaji ridhaa ya wazazi kuolewa wakati wavulana hawahitaji na kuonesha kwamba tofauti hiyo inatoa maana kwamba wasichana na wavulana hawatendewi sawa chini ya vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa na kuonesha ubaguzi na vinakiuka ibara ya 12 na 13 za Katiba ya nchi.
Hata hivyo, serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu ilikata rufani kupitia hukumu hiyo namba 204 la mwaka 2017 kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu lakini mwaka 2019 Mahakama ya Rufani ilimpatia tena ushindi Rebeca na kutoa mwaka mmoja sheria hiyo iwe imefanyiwa marekebisho. Lakini hadi leo serikali haijatekeleza amri ya mahakama.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED