Dk.Ndumbaro atumia Swalle Cup kuhamasisha wananchi kupiga kura

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 08:20 PM Nov 25 2024
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro.
Picha:Mtandao
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro amehimiza watanzania kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa ili kupata viongozi wa mitaa na vijiji kwa kuwa uchaguzi huo ndio muhimu zaidi kulinganisha na uchaguzi mwingine.

Dk. Ndumbaro ametoa rai hiyo wilayani Njombe wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Lupembe alipokuwa akifunga michuano ya Swalle Cup iliyokuwa ikifanyika katika kijiji cha Image ambapo pia amepigia chapuo Chama chake cha Mapinduzi (CCM) kwa wananchi kuwapa ridhaa wagombea wao kwa madai kuwa ndio chama kitakacholeta maendeleo.

"CCM ndio chama cha maendeleo na mashindano haya (Swalle Cup) ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ibara ya 243, juzi timu yetu ya taifa imefuzu Afcon ushindi ule ni utekelezaji wa Ilani ambayo inasisitiza serikali iimarishe michezo,sasa hicho ndio chama chenye Ilani waulizeni wengine Ilani zao ziko wapi," amesema Dk.Ndumbaro

Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Edwin Swalle na mdhamini wa michuano ya Swalle Cup amesema kutokana na jitihada kubwa za kuleta maendeleo zilizofanywa na serikali ndani ya jimbo hilo anaamini wananchi hawana shida na wanafahamu nini cha kufanya Novemba 27 mwaka huu na wapo tayari kuunga mkono chama cha mapinduzi ili kupata maendeleo wanayotarajia zaidi

Waziri Ndumbaro amefunga michuano ya Swalle cup na kushuhudia mtanange mkali fainali iliyozikutanisha timu ya Ikuna FC pamoja na Matembwe FC, ambapo dakika tisini zimekamilika kwa timu ya Ikuna FC kuibamiza mabao mawili kwa sifuri na kutawazwa kuwa bingwa michuano ya Swalle Cup msimu wa 2024.

4