CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kufunga Kampeni za Serikali za Mitaa leo kwa kishindo.
Kimesema watanzania watashuhudia mabadiliko kwa sababu CCM imejipanga kushinda uchaguzi huo.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla, aliyasema hayo jana wakati wa kampeni zilizofanyika jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam.
Alisema kuwa wakati wa ufunguzi wa kampeni, CCM ilisambaza viongozi wake katika mikoa mbalimbali na wakati wa kuzifunga leo watabadilishana, yeye anakwenda Morogoro aliko Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika na Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi atakwenda Dar es Salaam.
Makalla alijigamba kwamba katika siku sita za kampeni Mkoa wa Dar es Salaam, viongozi wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hawajaonekana mkoani humo.
"Siku zote sita sijaona kiongozi yeyote wa CHADEMA Dar es Salaam, tunatamba tu nimemwona (Freeman) Mbowe kaenda Songwe na Mbeya jana (juzi), nimemsikia akisema katika siku moja iliyobaki na mimi ninakwenda kwangu Machame (Kilimanjaro) kujitetea'. Tundu Lissu yeye mwisho ni Ikungi," alirusha kijembe kwa wanasiasa wenzake.
Makalla alisema CHADEMA hawajajiandaa kwa uchaguzi huo, akiwananga kuwa walipopewa fursa ya kutekeleza 4R, kipaumbele chao kikawa maandamano wakati CCM viongozi wake kuanzia chini hadi juu walikuwa kwa wananchi kuwaandaa kwa uchaguzi na kutatua kero zao.
Alisema mikutano yote aliyohudhuria mpaka sasa inatoa taswira na mwelekeo wa ushindi CCM.
Alisema kuwa juzi alikuwa Ukonga. Licha ya jua kali, mkutano ulikuwa mkubwa.
"Hakika kwa siku hizi sita Dar es Salaam kwetu ni siku sita za moto. Kampeni zimekuwa za kishindo na zinavyoendelea CCM itapata ushindi wa kishindo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu, alisema wenyeviti wao wakiingia keshokutwa wanadunda miaka mitano.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Zainab Khamis Shomari (MNEC), alikishukuru chama chake kwa kuwarejeshea wagombea imara.
“Shida ya watanzania ni maendeleo ambayo yamefanyika, ndio maana tukipita katika mikutano ya wenzetu tunashangaa ni mikutano au wanafanya shooting,” alidai.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Rehema Sombi, alisema kwa kutambua vijana ndio vuguvugu la maendeleo wapo kazini kuhakikisha vijana wote wanashinda kwa kishindo kesho.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED