Vijana washauriwa kubuni miradi inayoendana na sera

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 02:48 PM Nov 26 2024
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Sharif Ali Sharif
Picha: Mpigapicha Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Sharif Ali Sharif

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Sharif Ali Sharif amewataka vijana wa Kitanzania kubuni miradi inayoendana na sera za uwekezaji, ili kuwa sehemu ya kujenga uchumi wa nchi yao kwa vitendo.

Sharif alisema hayo jana, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Watendaji Wakuu Bora 100 wa Mwaka 2024, pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali zikiwamo kampuni zilizofanya vizuri mwaka huu.

“Vijana wana nafasi ya kufanya kampuni zao kutambulika katika soko la ndani na nje iwapo watatumia vyema mazingira mazuri ya uwekezaji ndani ya nchi yao,” alisema Sharif.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Eastern Star, Deogratius Kilawe, alisema dhumuni la kuandaa tuzo hizo ni  kusherehekea uongozi bora, kukuza uvumbuzi na kuhamasisha kizazi kijacho cha watendaji.

“Sisi waandaaji wa  tuzo hizi kwa kushirikiana wa The Global CEO Institute, lengo ni kukuza na  kuweka viwango, pamoja na kuleta mabadiliko chanya na matokeo ya kudumu katika tasnia na jumuiya tunazohudumia.,” alisema Kilawe.

Kilawe aliongeza kuwa ugawaji wa tuzo hizo umezingatia ubora wa kazi zilizofanywa na washiriki, huku baadhi ya washindi wakisema tuzo hizo zinatoa chachu kwa kampuni za Kitanzania, kuendelea kufanya vizuri kila mwaka, kwa kubuni bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko la kimataifa.

Kwenye tuzo hizo, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, ameshinda Tuzo ya Heshima katika Tuzo 100 Bora za Watendaji Afrika 2024, kutokana na mchango wake mkubwa katika uongozi na utoaji huduma.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuendeleza miundombinu ya Tanzania, kupitia dira ya kimkakati na ufanisi wa kiutendaji katika TARURA. Kama mpokeaji wa heshima hii, Seff anajiunga na kada ya wasomi wa viongozi wa Afrika wanaotambuliwa kwa ubora wao katika nyanja zao. 

Tuzo hiyo inaangazia uwezo wake wa kuhamasisha mabadiliko, kutekeleza masuluhisho ya kiubunifu, na kuzingatia viwango vya juu zaidi vya utawala.