MKUKI wataja mambo matano kukomesha ukatili wa kijinsia

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 03:39 PM Nov 26 2024
Waziri wa Katiba na Sheria Prof.Palamagamba Kabudi, akiteta jambo na viongozi wa MKUKI baada ya kuzindua kampeni ya Siku 16 za Kupinga uUkatili wa Kijinsia.
Picha: Elizabeth Zaya
Waziri wa Katiba na Sheria Prof.Palamagamba Kabudi, akiteta jambo na viongozi wa MKUKI baada ya kuzindua kampeni ya Siku 16 za Kupinga uUkatili wa Kijinsia.

WAZIRI wa Katiba na Sheria, jana alizindua Kampeni ya siku 16 za Uanaharakati wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia(MKUKI), iliyoratibiwa na Shirika la Wanawake na Maendeleo Afrika(WiLDAF).

Baada ya uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Mtandao huo, Dk.Monica Muhoja, aliwasilisha mbele ya Waziri, maombi matano kwa niaba ya MKUKI.

Maombi hayo ni pamoja na kutaka kufanyike maboresho kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu ili kusaidia kushughulikia masuala ya ukatili pamoja na kutunga sheria mahsusi ya kupambana na vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.

Dk.Monica alisema muda uliobaki kufikia ukomo wa malengo ya maendeleo endelevu ni mfupi, hivyo kuna haja ya kuimarisha sheria na sera ambazo zitaharakisha ufikiwaji wa malengo ambayo nchi imejiwekea ya kutokomeza ukatili ifikapo mwaka 2030.

“Sisi wana MKUKI, tumefanya utafiti kubainisha mapungufu kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia, tuko tayari kushirikiana ili tuwasilishe hizo tafiti na tufanye tafakuri ya pamoja na wataalamu wa Wizara ya Katiba na Sheria ili kubainisha mikakati na maeneo ya maboresho.

“Pia tuko tayari kwa umoja wetu kuendelea kufanya kazi na wizara hiyo ili kuharakisha mchakato wa maboresho ya sheria hizo kwa sababu muda uliobaki wa kufikia mwisho wa malengo ya maendeleo endelevu ni mfupi,”alisema Dk.Monica.

Eneo jingine ambalo waliomba ni kwa Mamlaka za usimamizi wa uchaguzi, kuandaa kanuni mahsusi za utekelezaji wa kifungu cha 135 cha sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge, madiwani kuhusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia kwenye uchaguzi.

“Hili limekuwa ni changamoto na kikwazo kikubwa katika ushiriki wa wanawake kwenye chaguzi hususani kwa wagombea, na tunataka liende sambamba na kuimarisha mifumo ya utoleaji taarifa na kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia kwenye uchaguzi na siasa,”alisema Dk.Monica.

Kadhalika, walitaka serikali iimarishe utekelezaji wa Mpangokazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA).

“Na hii kuanzia ngazi ya taifa mpaka vijiji na mitaa, tunaomba mamlaka husika, kutenga fedha za kutosha kuwezesha utekelezaji wa mpango huu, tunaziomba mamlaka zote kushiriki kikamilifu kwenye vikao vya kamati ikiwamo kuwasilisha taarifa muhimu zinazohitajika kuimarisha uratibu na ushughulikiwaji wa changamoto mbalimbali,”alisema Dk.Monica.

Walitaka masuala ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yajumuishwe katika ajenda za vikao vya ulinzi na usalama kwa ngazi zote.

“Pamoja na jitihada ambazo serikali inafanya kutokomeza vitendo vya ukatili, wanawake na watoto wengi wameendelea kuwa waathirika wa vitendo hivyo, pia kumekuwa na kulegalega kwa baadhi ya watendaji wa mamlaka husika katika kukabiliana na vitendo hivyo kwenye maeneo yao.

“Sisi tunaamini kwamba iwapo masuala hayo yataingizwa katika ajenda za vikao vya ulinzi na usalama ngazi zote, kutaleta msukumo mkubwa wa uwajibikaji katika kushughulikia matukio ya ukatil,” alisema Dk.Monica.

Pia, waliiomba serikali ifanyie maboresho sheria zinazogusa familia moja kwa moja ikiwamo sheria ya ndoa na mirathi.

“Kwa mfano Sheria za mirathi  na Sheria ya ndoa, zinabagua sana wanawake na mabinti hususani wajane, hizi zinachangia wengi kupata matatizo ya afya ya akili kwa sababu wanakuwa wanakandamizwa sana, kwa hiyo tuko pamoja na serikali kushirikiana kuhakikisha vitendo hivi vinakomeshwa.”

Waziri wa Katiba na Sheria, Prof.Palamagamba Kabudi, alisema vitendo vya ukatili ni aibu kwa nchi na havikubaliki na kwamba wizara yake iko tayari kukaa na wadau hao kupitia mapungufu yaliyopo katika sheria mbalimbali zinazochangia vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Kwa mfano Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ninashukuru kwamba mmefanya utafiti na kubainisha mapungufu, ni kiri kwamba ni kwa muda mrefu hatujafanyia maboresho katika eneo hili, kuna haja tulifanyie kazi,” alisema Prof. Kabudi.