KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), DK. Emmanuel Nchimbi amewaonya wagombea wa chama hicho watakaoshinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kutotumia madaraka yao kuwaumiza wananchi.
Amesema chama hakitakuwa na huruma kwa kiongozi wa namna hiyo na kwamba atachukuliwa hatua kali ikiwemo kutenguliwa.
Amesema hayo leo wilayani Temeke katika Jimbo la Mbagala wakati akifunga kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
"Tunawategemea nyie wagombea mtakaopitishwa na kuwa wagombea wa vijiji, mitaa na vitongoji mkawatumikie wananchi na siyo kwenda kutumia madaraka yenu kuwaumiza wananchi. Chama hakitavumilia wala kuwa na huruma kwa yoyote," amesema Dk. Nchimbi.
Kadhalika, amewataka Watanzania kuwachagua wagombea wa CCM ili kujihakikishia maendeleo, amani, utulivu katika maeneo yao.
Amesema CCM chini ya mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa na kuleta maendeleo kwa wananchi hali inayoyavutia mataifa mengine duniani kutaka kuja kujifunza.
"Kesho watanzania nendeni mkakichague CCM kwa sababu hakipendi ugomvi, chama chenye kiu ya maendeleo, kinapenda amani pamoja na kuwaheshimu wananchi," amesema Dk. Nchimbi.
Aidha, amewataka Watanzania kusimama kidete kukataa kufarakana bali waenzi misingi mizuri iliyoachwa na watangulizi.
Vilevile, amewapongeza Watanzania kwa kufanya kampeni kwa amani, utulivu kwa sababu hakuna mtanzania aliyeripotiwa amefariki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED