KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad amewataka wananchi kuendelea kuitunza amani iliyoko, kwani ndiyo kichocheo kikubwa cha utalii nchini.
Kamishna Hamad aliyasema hayo katika uzinduzi wa operesheni maalum ya kuzuia na kukabiliana na matukio ya uhalifu na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani ambapo uzinduzi huo umefanyika Shehia ya Kwamtipura, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema sekta ya utalii ni muhimu katika kuchochea maendeleo makubwa nchini na inamgusa kila mmoja katika jamii, hivyo endapo nchi itakuwa haina amani, itachangia watalii kutokuja na kuathiri mapato ambayo kwa kiasi kikubwa yanategemea shughuli za kitalii.
Kamishna Hamad alisema kupitia uzinduzi wa Filamu ya Royal Tour iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan imeongeza watalii nchini.
Alsisitiza kuwa ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha amani inadumishwa ili kutoa fursa ya watalii hao kufanya utalii nchini.
Kamishna Hamad alisema madereva wa bodaboda wanapaswa kuwa sehemu ya kudumisha usalama na sio chanzo cha uhalifu.
Alisema kumekuwa na matukio kadhaa yanayohusisha madereva hao kufanya unyang'anyi, kusambaza dawa za kulevya na hata kusafirisha wahalifu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Aliwaagiza masheha kupita nyumba kwa nyumba ili kuwabaini wahalifu na hatua za kisheria kuchukuliwa bila kumwonea mtu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu, alisema takribani watuhumiwa 50 walikamatwa katika operesheni ya kuzuia mapanga iliyozinduliwa mwezi Mei, mwaka huu, wanatumikia adhabu za vifungo jela na kuahidi kuendelea kuisimamia ili kuhakikisha wahalifu wanadhibitiwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED