Rais wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Dk.Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, kilichotokea usiku wa kuamkia leo huko nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Rais Samia kwenye ukurasa wake wa Instagram ameandika; "Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, kilichotokea usiku wa kuamkia leo Novemba 27, 2024."
Aidha amesema "Ninatoa salamu za pole kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote"
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED